Malaki 4 - Swahili Revised Union VersionSiku kuu ya Bwana 1 Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuri; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema BWANA wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi. 2 Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawachomozea, likiwa na uwezo wa kuponya katika miale yake; nanyi mtatoka nje, na kuchezacheza kama ndama watokapo mazizini. 3 Nanyi mtawakanyaga waovu; maana watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu; katika siku ile niifanyayo, asema BWANA wa majeshi. 4 Ikumbukeni Torati ya Musa, mtumishi wangu, niliyomwamuru huko Horebu kwa ajili ya Israeli wote, naam, amri na hukumu. 5 Angalieni, nitawatumia Eliya nabii, kabla siku ile ya BWANA, iliyo kuu na ya kuogofya haijafika. 6 Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya