Isaya 36 - Swahili Revised Union VersionSenakeribu atishia Yerusalemu 1 Ikawa, katika mwaka wa kumi na nne wa kutawala kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa. 2 Mfalme wa Ashuru akamtuma amiri toka Lakishi pamoja na jeshi kubwa kwenda hadi Yerusalemu kwa mfalme Hezekia. Naye akasimama karibu na mfereji wa bwawa la juu, lililo katika njia kuu ya kuuendea Uwanda wa Dobi. 3 Wakamtokea Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika kumbukumbu. 4 Yule kamanda akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kwamba mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia? 5 Nasema, mashauri yako, na nguvu zako kwa vita, ni maneno yasiyo na maana; basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi? 6 Tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliovunjika, yaani, Misri, ambayo, mtu akitegemea juu yake, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio. 7 Lakini ukiniambia, Tunamtumaini BWANA, Mungu wetu, je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake mlimoinuka, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii? 8 Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao. 9 Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa afisa mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi? 10 Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la BWANA? BWANA ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza. 11 Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule kamanda, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa watu wote walio ukutani. 12 Lakini yule kamanda akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma niseme, maneno haya kwa bwana wako na kwako wewe? Hakunituma pia kwa watu hawa wanaokaa ukutani, wanaokabiliwa na tisho la kula mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi? 13 Kisha yule kamanda akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akisema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru. 14 Mfalme asema hivi; Hezekia asiwadanganye, kwa maana hataweza kuwaokoa; 15 wala msimwache Hezekia kuwatia moyo wa kumtumaini BWANA; akisema, BWANA bila shaka atatuokoa, mji huu hautatiwa katika mkono wa mfalme wa Ashuru. 16 Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie, mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya kisima chake mwenyewe; 17 hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu. 18 Jihadharini, Hezekia asije akawadanganya, akisema, BWANA atatuokoa. Je! Kati ya miungu ya mataifa, kuna yeyote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka kwa mkono wa mfalme wa Ashuru? 19 Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je! Wameiokoa Samaria kutoka kwa mkono wangu? 20 Katika miungu yote ya nchi hizi ni nani waliookoa nchi yao kutoka kwa mkono wangu, hata BWANA auokoe Yerusalemu kutoka kwa mkono wangu? 21 Lakini watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana ilikuwa amri ya mfalme, kwamba, Msimjibu neno. 22 Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu mwenye kuandika kumbukumbu, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zikiwa zimeraruliwa, wakamwambia Hezekia maneno ya yule kamanda. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya