Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Isaya 25 - Swahili Revised Union Version


Sifa kwa kukombolewa katika udhalimu

1 Ee BWANA, wewe u Mungu wangu; Nitakutukuza na kulihimidi jina lako; Kwa kuwa umetenda mambo ya ajabu, Mashauri ya kale, kwa uaminifu na kweli.

2 Kwa sababu umefanya mji kuwa ni rundo; Mji wenye boma kuwa ni magofu; Jumba la wageni kuwa si mji; Hautajengwa tena milele.

3 Kwa hiyo watu walio hodari watakutukuza, Miji ya mataifa yatishayo itakuogopa.

4 Maana umekuwa ngome ya maskini, Ngome ya mhitaji katika dhiki yake, Mahali pa kukimbilia wakati wa tufani, Na kivuli wakati wa joto; Wakati kishindo cha watu wakatili kilipokuwa, Kama dhoruba ipigayo ukuta.

5 Kama vile joto katika mahali pakavu Utaushusha mshindo wa wageni; Kama ilivyo joto kwa kivuli cha wingu, Wimbo wa hao watishao utashushwa.

6 Na katika mlima huu BWANA wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana.

7 Naye katika mlima huu atauharibu utando uliowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote.

8 Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana BWANA amenena hayo.

9 Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye BWANA tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.

10 Kwa maana mkono wa BWANA utatulia katika mlima huu, na Moabu atakanyagwa chini huko aliko, kama vile majani makavu yakanyagwavyo katika maji machafu.

11 Naye atanyosha mikono yake katikati yake, kama vile aogeleaye anyoshavyo mikono yake ili aogelee, naye atashusha kiburi chake, pamoja na hila za mikono yake.

12 Na boma la ngome ya kuta zako ameliinamisha, na kulilaza chini, na kulitupa chini hadi mavumbini.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo