Isaya 18 - Swahili Revised Union VersionUtabiri juu ya Kushi 1 Ole wa nchi ya uvumi wa mabawa, Iliyoko mbali kupita mito ya Kushi; 2 Ipelekayo wajumbe wake kwa njia ya bahari, Na katika vyombo vya manyasi juu ya maji. Nendeni, wajumbe wepesi, kwa watu warefu, laini; Watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa; Taifa la wenye nguvu, wakanyagao watu, Ambao mito inakata nchi yao. 3 Enyi watu mkaao katika ulimwengu wote, na wenyeji wa dunia, bendera ikiinuliwa milimani, angalieni; na wakipiga tarumbeta, sikieni. 4 Maana BWANA ameniambia hivi, Mimi nitatulia, na kuangalia katika makazi yangu, kama wakati wa mwangaza mweupe wa jua kali, mfano wa wingu la umande katika joto la mavuno. 5 Maana kabla ya mavuno, maua yaangukapo, na maua yakawa zabibu zianzazo kuiva, ndipo atakapoyakata matawi kwa miundu, na kuviondoa vitawi vilivyopanuka na kuvikata. 6 Wote pamoja wataachiwa ndege wakali wa milimani, na wanyama wa nchi; ndege wakali watakaa juu yao wakati wa jua, na wanyama wote wa nchi watakaa juu yao wakati wa baridi. 7 Wakati huo BWANA wa majeshi ataletewa hidaya na watu warefu, laini; Watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa; Taifa la wenye nguvu, wakanyagao watu, Ambao mito inagawanya nchi yao; Mpaka mahali pa jina la BWANA wa majeshi, mlima Sayuni. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya