Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Isaya 15 - Swahili Revised Union Version


Utabiri juu ya Moabu

1 Ufunuo juu ya Moabu. Maana katika usiku mmoja Ari wa Moabu umeharibiwa kabisa na kuangamizwa; maana katika usiku mmoja Kiri wa Moabu umeharibiwa kabisa na kuangamizwa.

2 Wanapanda juu hata Bayithi na Diboni, mpaka mahali palipo juu ili walie; juu ya Nebo na juu ya Medeba Wamoabi wanalia; Wana upaa juu ya vichwa vyao vyote; kila ndevu zimenyolewa.

3 Wanajivika nguo za magunia katika njia kuu zao; juu ya madari yao, na katika mitaa yao, kila mtu analia, anamwaga machozi.

4 Heshboni analia na Eleale; mpaka Yahasa sauti ya kulia kwao inasikiwa; hata watu wa Moabu waliovaa silaha wanapiga kelele sana kwa sababu hiyo; nafsi yake inatetemeka ndani yake.

5 Moyo wangu unamlilia Moabu; wakuu wake wanakimbilia Soari kama ndama wa miaka mitatu; kwa maana wanapanda mbavu za Luhithi wakilia; maana katika njia iendayo hata Horonaimu wanatoa kilio cha maangamizi.

6 Kwa maana maji ya Nimrimu yamekuwa mahali palipoharibika, kwa kuwa majani yamekauka, miche imenyauka, majani mabichi yamekoma.

7 Kwa hiyo vitu walivyojipatia tele, na akiba yao, wanavichukua hadi kijito cha Mierebi.

8 Maana kilio hicho kimezunguka mipaka ya Moabu, malalamiko yao yamefika hata Eglaimu, na malalamiko yao hata Beer-Elimu.

9 Maana maji ya Dimoni yamejaa damu; maana ninatayarisha msiba mpya juu ya Dimoni, simba juu ya watu wa Moabu waliokimbia, na juu ya mabaki yao.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo