Yule nyama akakamatwa pamoja na yule nabii wa uongo aliyeonyesha vitambulisho mbele yake. (Ni kwa njia ya vitambulisho vile aliwadanganya wale waliopigwa chapa ya yule nyama na wale walioabudu sanamu yake.) Nyama yule pamoja na nabii wa uongo wakatupwa wangali wazima katika ziwa la moto munamowaka mawe ya kiberiti.
Kisha nikaona viti vya kifalme na watu waliokuwa wakiikaa juu yao, wakapewa uwezo wa kuhukumu. Nikaona vilevile roho za wale waliochinjwa kwa sababu ya kutangaza ukweli ulioshuhudiwa na Yesu na Neno la Mungu. Watu wale hawakumwabudu yule nyama wa ajabu, wala sanamu yake, wala hawakupigwa chapa yake juu ya paji za nyuso zao, au juu ya mikono yao. Nao wakafufuka na kutawala pamoja na Kristo muda wa miaka elfu moja.