Nitafanya hivyo kwa sababu Solomono ameniacha, akaabudu miungu ya kigeni: Astaroti mungu wa Wasidoni, Kemosi mungu wa Wamoabu, na Milkomu mungu wa Waamoni. Solomono ameniasi, ametenda maovu mbele yangu. Hakutii masharti yangu na maagizo yangu kama Daudi baba yake alivyofanya.