Rafiki yangu, tumeumbwa kumwabudu na kumsifu Mungu, na tukifanya hivyo, tunapata baraka pia. Kumbuka ile stori katika Matendo 16:25-26, usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wanaomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu gerezani, ghafula, tetemeko kubwa la ardhi likatikisa msingi wa gereza, milango ikafunguka, na minyororo ya wafungwa ikafunguka. Hili linatuonyesha nguvu ya sifa.
Mimi nasema hivi, kama waumini, tukiuelewa uzito wa sifa, tungemwimbia Bwana wakati wote. Sauti yangu iweje haijalishi; jina la Yesu linastahili kutukuzwa kila wakati. Tukitambua ukuu wake na kutangaza nguvu zake, milango itafunguka na minyororo itavunjika maishani mwetu.
Ni nani awezaye kutaja matendo ya Mwenyezi-Mungu? Ni nani awezaye kumsifu kama anavyostahili?
Maana Mwenyezi-Mungu ni mkuu, anasifika sana anastahili kuheshimiwa kuliko miungu yote.
Utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, utukusanye pamoja kutoka kwa mataifa, tupate kulisifu jina lako takatifu, na kuona fahari juu ya sifa zako.
Lakini wakati waja, tena umekwisha wasili, ambapo wenye kuabudu wa kweli watamwabudu Baba katika roho na ukweli. Maana Baba anawataka watu wanaomwabudu namna hiyo.
Nitakushukuru Mungu kwa moyo wangu wote; nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu. Wanaokujua wewe, ee Mungu hukutegemea, wewe Mwenyezi-Mungu huwatupi wakutafutao. Mwimbieni sifa Mwenyezi-Mungu akaaye Siyoni. Yatangazieni mataifa mambo aliyotenda! Mungu hulipiza kisasi kwa umwagaji damu; kamwe hasahau kilio cha wanaoonewa. Unirehemu, ee Mwenyezi-Mungu! Ona mateso ninayoteswa na wanaonichukia; wewe waninyakua kutoka nguvu za kifo, nisimulie sifa zako mbele ya watu wa Siyoni, nipate kushangilia kwa sababu umeniokoa. Watu wa mataifa wametumbukia katika shimo walilochimba, wamenaswa miguu katika wavu waliouficha. Mwenyezi-Mungu amejionesha alivyo; ametekeleza hukumu. Watu waovu wamenaswa kwa matendo yao wenyewe. Waovu wataishia kuzimu; naam, mataifa yote yanayomsahau Mungu. Lakini fukara hawatasahauliwa daima; tumaini la maskini halitapotea milele. Inuka, ee Mwenyezi-Mungu! Usimwache binadamu ashinde. Uyakusanye mataifa mbele yako, uyahukumu. Nitafurahi na kushangilia kwa sababu yako; nitaliimbia sifa jina lako, ewe Mungu Mkuu.
Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu tambiko ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa kwa midomo inayoliungama jina lake.
Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na Zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu.
Yeye ni fahari yenu; ndiye Mungu wenu ambaye amewatendea haya mambo makubwa na ya kutisha mliyoyaona kwa macho yenu wenyewe.
Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini ya dunia na baharini – viumbe vyote ulimwenguni – vikisema: “Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo, iwe sifa na heshima na utukufu na enzi, milele na milele.”
wakasema kwa sauti kuu: “Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, utukufu na sifa.”
Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu; tegemeo la moyo wangu limo kwake. Amenisaidia nami nikashangilia kwa moyo; kwa wimbo wangu ninamshukuru.
Heri watu wanaojua kukushangilia, wanaoishi katika mwanga wa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu.
Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena Mungu, aliye msaada wangu na Mungu wangu.
Basi, watu wakapiga kelele huku mabaragumu yanapigwa. Watu waliposikia sauti ya mabaragumu walipiga kelele kubwa, na kuta za mji zikaanguka chini kabisa. Mara watu wakauvamia mji, kila mmoja kutoka mahali aliposimama, wakauteka.
Hapo, Mose pamoja na Waisraeli wakamwimbia Mwenyezi-Mungu wimbo huu, “Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu kwani ameshinda kwa fahari, farasi na mpandafarasi wake amewatosa baharini.
Enyi watu wote, pigeni makofi! Msifuni Mungu kwa sauti za shangwe! Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu, anatisha. Yeye ni Mfalme mkuu wa ulimwengu wote.
Mwenyezi-Mungu, ni mkuu; astahili kusifiwa sana katika mji wake na mlima wake mtakatifu.
Anayenipa shukrani kama tambiko yake, huyo ndiye anayeniheshimu; yeyote anayedumu katika njia yangu, huyo ndiye nitakayemwokoa.”
Niko thabiti moyoni, ee Mungu, naam, niko thabiti moyoni; nitaimba na kukushangilia! Amka, ee nafsi yangu! Amkeni, enyi kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko! Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa; nitakuimbia sifa kati ya mataifa.
Fadhili zako ni bora kuliko maisha, nami nitakusifu kwa mdomo wangu. Nitakushukuru maisha yangu yote; nitainua mikono yangu na kukuomba.
Enyi watu wote duniani mshangilieni Mungu! Umetupima, ee Mungu, umetujaribu kama madini motoni. Umetuacha tunaswe wavuni; umetubebesha taabu nzito. Umewaacha watu watukanyage; tumepitia motoni na majini. Lakini sasa umetuleta kwenye usalama. Nitakuja nyumbani kwako na sadaka za kuteketezwa, nitakutimizia nadhiri zangu, nilizotamka na kukuahidi mimi mwenyewe nilipokuwa taabuni. Nitakutolea sadaka za kuteketezwa nononono, tambiko za kuteketezwa za kondoo madume; nitatoa sadaka za ng'ombe na mbuzi. Enyi mnaomcha Mungu, njoni nyote mkasikilize, nami nitawasimulieni aliyonitendea. Mimi nilimlilia msaada kwa sauti, sifa zake nikazitamka. Kama ningalinuia maovu moyoni, Mwenyezi-Mungu hangalinisikiliza. Lakini kweli Mungu amenisikiliza; naam, amesikiliza maneno ya sala yangu. Imbeni juu ya utukufu wa jina lake, mtoleeni sifa tukufu!
Ni vema kukushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kuliimbia sifa jina lako, ee Mungu Mkuu. Wewe umenipa nguvu kama nyati; umenimiminia mafuta ya kuburudisha. Kwa macho nimeona maadui zangu wameshindwa; nimesikia kilio chao watendao maovu. Waadilifu hustawi kama mitende; hukua kama mierezi ya Lebanoni! Kama miti iliyopandwa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu, hustawi katika nyua za Mungu wetu; huendelea kuzaa matunda hata uzeeni; daima wamejaa utomvu na wabichi; wapate kutangaza kwamba Mwenyezi-Mungu ni mnyofu, Mwamba wangu, kwake hamna upotovu. Ni vema kutangaza fadhili zako asubuhi, na uaminifu wako nyakati za usiku,
Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote! Yaambieni mataifa: “Mwenyezi-Mungu anatawala! Ameuweka ulimwengu imara, hautatikisika. Atawahukumu watu kwa haki!” Furahini enyi mbingu na dunia! Bahari na ivume pamoja na vyote vilivyomo! Furahini enyi mashamba na vyote vilivyomo! Ndipo miti yote misituni itaimba kwa furaha, mbele ya Mwenyezi-Mungu anayekuja; naam, anayekuja kuihukumu dunia. Ataihukumu dunia kwa haki, na mataifa kwa uaminifu wake. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu na kulisifu jina lake. Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu.
Pitieni milango ya hekalu lake kwa shukrani, ingieni katika nyua zake kwa sifa. Mshukuruni na kulisifu jina lake.
Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu; nafsi yangu yote ilisifu jina lake takatifu! Yeye hatuadhibu kama tunavyostahili; hatulipizi kadiri ya uovu wetu. Kama vile anga lilivyo juu mbali na dunia, ndivyo ulivyo mwingi wema wake kwa watu wanaomcha. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo azitengavyo dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba amhurumiavyo mwanawe, ndivyo Mwenyezi-Mungu awahurumiavyo wote wamchao. Mungu ajua mfumo wa nafsi zetu; ajua kwamba sisi ni mavumbi. Walakini binadamu, maisha yake ni kama nyasi tu; huchanua kama ua shambani: Upepo huvuma juu yake nalo latoweka; na mahali lilipokuwa hapaonekani tena. Lakini fadhili za Mwenyezi-Mungu hudumu milele, kwa wale wote wanaomheshimu; na wema wake wadumu vizazi vyote, kwa wote wanaozingatia agano lake, wanaokumbuka kutii amri zake. Mwenyezi-Mungu ameweka kiti chake cha enzi mbinguni; yeye anatawala juu ya vitu vyote. Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu! Usisahau kamwe wema wake wote.
Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, tangazeni ukuu wake; yajulisheni mataifa mambo aliyotenda! Alimthibitishia Yakobo ahadi yake, alimhakikishia Israeli agano hilo la milele. Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani, nayo itakuwa mali yenu wenyewe.” Watu wa Mungu walikuwa wachache; hawakuwa maarufu, tena walikuwa wageni nchini Kanaani. Walitangatanga kutoka taifa hadi taifa; kutoka nchi moja hadi nchi nyingine. Lakini Mungu hakuruhusu mtu awadhulumu; kwa ajili yao aliwaonya wafalme: “Msiwaguse wateule wangu; msiwadhuru manabii wangu!” Mungu alizusha njaa nchini mwao, akaharibu chakula chao chote. Lakini aliwatangulizia mtu mmoja, Yosefu aliyekuwa ameuzwa utumwani. Walimfunga miguu kwa minyororo, na shingoni kwa nira ya chuma, Muda si muda alichotabiri kilitimia. neno la Mwenyezi-Mungu lilimdhibiti. Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa; simulieni matendo yake ya ajabu!
Haleluya! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele!
Sio sisi, ee Mwenyezi-Mungu, sio sisi; bali wewe peke yako utukuzwe, kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako.
Enyi mataifa yote, msifuni Mwenyezi-Mungu! Enyi watu wote mhimidini! Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu; uaminifu wake Mwenyezi-Mungu wadumu milele! Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kwa moyo wangu wote, naimba sifa zako mbele ya miungu. Ninasujudu kuelekea hekalu lako takatifu; nalisifu jina lako, kwa sababu ya fadhili zako na uaminifu wako; kwa sababu umeweka jina lako na neno lako juu ya kila kitu.
Nitakutukuza, ee Mungu wangu na mfalme wangu; nitalitukuza jina lako daima na milele. Viumbe vyako vyote vitakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, nao waaminifu wako watakutukuza. Watasema juu ya utukufu wa ufalme wako, na kutangaza juu ya nguvu yako kuu, ili kila mtu ajue matendo yako makuu, na fahari tukufu ya ufalme wako. Ufalme wako ni ufalme wa milele; mamlaka yako yadumu vizazi vyote. Mwenyezi-Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake zote, ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu huwategemeza wote wanaoanguka; huwainua wote waliokandamizwa. Viumbe vyote vinakutazama kwa hamu, nawe wavipa chakula chao kwa wakati wake. Waufumbua mkono wako kwa ukarimu, watosheleza mahitaji ya kila kiumbe hai. Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu katika njia zake zote; ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu yuko karibu na wote wanaomwomba, wote wanaomwomba kwa moyo mnyofu. Huwapatia mahitaji yao wote wanaomcha; husikia kilio chao na kuwaokoa. Nitakutukuza kila siku; nitalisifu jina lako daima na milele. Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wanaompenda; lakini atawaangamiza waovu wote. Nitatangaza sifa za Mwenyezi-Mungu; viumbe vyote vilisifu jina lake takatifu, milele na milele. Mwenyezi-Mungu ni mkuu, astahili sifa nyingi; ukuu wake hauwezi kuchunguzika.
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu! Mwenyezi-Mungu atawala milele, Mungu wako, ee Siyoni, ni mfalme vizazi vyote! Msifuni Mwenyezi-Mungu! Nitamsifu Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote; nitamwimbia Mungu wangu muda wote niishipo.
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Jinsi gani ilivyo vizuri kumwimbia sifa Mungu wetu! Yeye ni mwema na astahili kuimbiwa sifa.
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mungu katika patakatifu pake; msifuni katika mbingu zake kuu. Msifuni kwa sababu ya matendo yake makuu; msifuni kwa ajili ya utukufu wake mkuu. Msifuni kwa mlio wa tarumbeta; msifuni kwa zeze na kinubi! Msifuni kwa ngoma na kucheza; msifuni kwa filimbi na banjo! Msifuni kwa kupiga matoazi. Msifuni kwa matoazi ya sauti kubwa. Kila kiumbe hai kimsifu Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu na uwezo, yeye mwenyewe ndiye anayeniokoa. Yeye ni Mungu wangu nami nitamsifu, ni Mungu wa baba yangu nami nitamtukuza.
“Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa, ee Mwenyezi-Mungu, nitaliimbia sifa jina lako.
Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote. Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu. Yatangazieni mataifa utukufu wake, waambieni watu wote matendo yake ya ajabu. Maana Mwenyezi-Mungu ni mkuu, anasifika sana anastahili kuheshimiwa kuliko miungu yote.
Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele!
Ndipo Daudi akamtukuza Mwenyezi-Mungu mbele ya mkutano wote, akisema: “Utukuzwe milele na milele, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yetu Israeli. Ukuu ni wako, ee Mwenyezi-Mungu, una nguvu, utukufu, ushindi na enzi. Vyote vilivyoko mbinguni na duniani ni vyako. Ee Mwenyezi-Mungu, ufalme ni wako, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako, vyote wavitawala. Uwezo na nguvu vimo mkononi mwako, nawe wawakuza uwapendao, na huwaimarisha wote. Sasa ee Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.
Waimbaji, huku wakifuatiwa na sauti linganifu za tarumbeta, matoazi na vyombo vingine vya muziki, walimsifu Mwenyezi-Mungu wakiimba: “Maana yeye ni mwema, na fadhili zake zadumu milele.” Wakati huo nyumba ya Mwenyezi-Mungu ilijazwa wingu. Nao makuhani walishindwa kuhudumu humo kwa sababu ya wingu hilo, maana utukufu wa Mwenyezi-Mungu uliijaza nyumba ya Mungu.
Baada ya kushauriana na watu, mfalme alichagua wanamuziki fulani, akawaagiza wajivike mavazi yao rasmi kisha watangulie mbele ya jeshi, wakiimba: “Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, maana fadhili zake zadumu milele!” Wakati walipoanza kuimba na kusifu, Mwenyezi-Mungu aliwavuruga akili wanajeshi wa Amoni, Moabu na wa Mlima Seiri waliokuja kupigana na Yuda. Na wanajeshi hao wakashindwa.
Waliimba kwa kupokezana, wakimsifu na kumtukuza Mwenyezi-Mungu: “Kwa kuwa yu mwema, fadhili zake kwa Israeli zadumu milele.” Watu wote walipaza sauti kwa nguvu zao zote, wakamsifu Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya kuanza kujengwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
Walawi, yaani: Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabuea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakawaambia watu; “Simameni na kumsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Msifuni milele na milele! Na watu walisifu jina lako tukufu, ambalo hutukuka kuliko baraka na sifa zote.” Ezra akaomba kwa sala ifuatayo: “Wewe peke yako ndiwe Mwenyezi-Mungu; ndiwe uliyefanya mbingu na jeshi lake lote, dunia na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo; nawe ndiwe unayevihifadhi hai, na jeshi lote la mbinguni lakuabudu wewe.
Akasema, “Uchi nilikuja duniani, uchi nitaondoka duniani; Mwenyezi-Mungu amenipa, Mwenyezi-Mungu amechukua; litukuzwe jina lake Mwenyezi-Mungu.”
Siku hiyo mtasema: “Mshukuruni Mwenyezi-Mungu mwombeni kwa jina lake. Yajulisheni mataifa matendo yake, tangazeni kuwa jina lake limetukuka. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa kwa kuwa ametenda mambo makuu; haya na yajulikane duniani kote.
Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe Mungu wangu; nitakutukuza na kulisifu jina lako, kwa maana umetenda mambo ya ajabu; waitekeleza kwa uaminifu na kweli mipango uliyoipanga tangu zamani.
Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya! Dunia yote iimbe sifa zake: Bahari na vyote vilivyomo, nchi za mbali na wakazi wake;
niwape wale wanaoomboleza katika Siyoni taji la maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya moyo mzito. Nao wataitwa mialoni madhubuti, aliyopanda Mwenyezi-Mungu kuonesha utukufu wake.
Nitasimulia fadhili za Mwenyezi-Mungu; nitataja matendo yake yote yastahiliyo sifa, kwa sababu ya yote aliyotutendea, wema wake mkuu aliowapa Waisraeli kwa huruma yake, kadiri ya wingi wa fadhili zake.
Mwimbieni Mwenyezi-Mungu; msifuni Mwenyezi-Mungu, kwani ameyaokoa maisha ya mhitaji, kutoka mikononi mwa watu waovu.
Hata kama mitini isipochanua maua, wala mizabibu kuzaa zabibu; hata kama mizeituni isipozaa zeituni, na mashamba yasipotoa chakula; hata kama kondoo wakitoweka zizini, na mifugo kukosekana mazizini, mimi nitaendelea kumfurahia Mwenyezi-Mungu nitamshangilia Mungu anayeniokoa.
Shangilieni sana enyi watu wa Siyoni! Paazeni sauti, enyi watu wa Yerusalemu! Tazama, mfalme wenu anawajieni, anakuja kwa shangwe na ushindi! Ni mpole, amepanda punda, mwanapunda, mtoto wa punda.
Makundi ya watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti: “Sifa kwa Mwana wa Daudi! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Sifa kwa Mungu juu!”
Hivyo wakamwambia, “Je, husikii wanachosema?” Yesu akawajibu, “Naam, nasikia! Je hamjapata kusoma Maandiko haya? ‘Kwa vinywa vya watoto wadogo na wachanga wajipatia sifa kamili.’”
Naye Maria akasema, “Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema: “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu anaowafadhili!”
Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona; wakawa wanasema: “Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!”
Lakini wakati waja, tena umekwisha wasili, ambapo wenye kuabudu wa kweli watamwabudu Baba katika roho na ukweli. Maana Baba anawataka watu wanaomwabudu namna hiyo. Mungu ni roho, na watu wanaomwabudu lazima wamwabudu kwa Roho na ukweli.”
Waliendelea kukutana pamoja kila siku hekaluni. Lakini wakati wa kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula hicho kwa furaha na moyo mkunjufu. Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa.
Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza. Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana.
ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Kwa hiyo nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa. Nitaziimba sifa za jina lako.”
Ndugu, tuseme nini, basi? Mnapokutana pamoja, mmoja aimbe wimbo, mwingine atoe mafundisho, mwingine awe na ufunuo kutoka kwa Mungu, mwingine atumie kipaji cha kusema kwa lugha ngeni na mwingine afafanue yanayosemwa. Yote yawe kwa ajili ya kulijenga kanisa.
Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.
Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu ambayo ametujalia katika Mwanae mpenzi!
Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu. Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na Zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu. Upendo uongoze maisha yenu kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama tambiko yenye harufu nzuri na sadaka impendezayo Mungu. Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
Maisha yenu yatajazwa mambo yote yaliyo kweli bora, ambayo Yesu Kristo mwenyewe anaweza kuwajalieni, kwa ajili ya utukufu na sifa ya Mungu.
Hatimaye, ndugu zangu, zingatieni mambo mema na yanayostahili kusifiwa; mambo ya kweli na bora; mambo ya haki, safi, ya kupendeza na ya heshima.
Na kwa furaha mshukuruni Baba, aliyewawezesha nyinyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale aliyowawekea watu wake katika ufalme wa mwanga.
Ujumbe wa Kristo na ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani. Na, kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake.
Furahini daima, salini kila wakati na kuwa na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.
Kwake yeye aliye Mfalme wa milele, asiyekufa, asiyeonekana na aliye Mungu pekee – kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina.
kama asemavyo: “Ee Mungu, nitawasimulia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao.”
Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu. Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na tambiko hizo zote zingekoma. Yeye ametufungulia njia mpya, njia ya uhai, kupitia lile pazia, yaani mwili wake mwenyewe. Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa kutokana na dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.
Sisi basi, na tushukuru, kwani tunapokea ufalme usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu;
Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Ametujalia tumaini lenye uhai,
Lakini nyinyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu.
Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina.
Lakini endeleeni kukua katika neema na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu uwe kwake, sasa na hata milele! Amina.
Oneni, basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu.
Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta nyinyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake, kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina.
akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina.
wakasema kwa sauti kuu: “Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, utukufu na sifa.” Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini ya dunia na baharini – viumbe vyote ulimwenguni – vikisema: “Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo, iwe sifa na heshima na utukufu na enzi, milele na milele.”
wakisema: “Tunakushukuru ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu, uliyeko na uliyekuwako! Maana umetumia nguvu yako kuu, ukaanza kutawala!
Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikisema: “Sasa umefika ukombozi na nguvu na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake! Maana yule aliyewashtaki ndugu zetu mbele ya Mungu ametupwa chini. Naam, ametupwa chini huyo anayewashtaki usiku na mchana. Ndugu zetu wamemshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno waliloshuhudia; maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana, wakawa tayari kufa.
Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu na wa Mwanakondoo: “Bwana Mungu Mwenye Nguvu, matendo yako ni makuu na ya ajabu mno! Ewe Mfalme wa mataifa, njia zako ni za haki na za kweli! Bwana, ni nani asiyekucha wewe? Nani asiyelitukuza jina lako? Wewe peke yako ni Mtakatifu. Mataifa yote yatakujia na kukuabudu maana matendo yako ya haki yamedhihirishwa.”
Baada ya hayo nikasikia kitu kama sauti kubwa ya umati wa watu wengi mbinguni ikisema, “Asifiwe Mungu! Ukombozi, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!
Kisha, kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: “Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.” Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, “Asifiwe Mungu! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Nguvu ametawala!
Njoni tumwimbie Mwenyezi-Mungu, tumshangilie mwamba wa wokovu wetu! Kwa miaka arubaini nilichukizwa nao, nikasema: ‘Kweli, hawa ni watu waliopotoka! Hawajali kabisa njia zangu!’ Basi, nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko!’” Twende mbele zake na shukrani; tumshangilie kwa nyimbo za sifa.
Dunia yote imshangilie Mwenyezi-Mungu; imsifu kwa nyimbo na vigelegele. Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa shangwe, msifuni kwa sauti tamu za zeze. Mpigieni vigelegele Mwenyezi-Mungu mfalme wetu, mshangilieni kwa tarumbeta na sauti ya baragumu.
Mwenyezi-Mungu atawala milele, Mungu wako, ee Siyoni, ni mfalme vizazi vyote! Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Waisraeli wote walipoona moto ukishuka kutoka mbinguni na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulijaa katika nyumba walisujudu nyuso zao zikifika mpaka sakafuni, wakamwabudu na kumshukuru Mwenyezi-Mungu wakisema, “Kwa kuwa ni mwema, fadhili zake zadumu milele.”
Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaza sauti wakisema: “Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli.”
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya; msifuni katika kusanyiko la waaminifu! Furahi ee Israeli kwa sababu ya Muumba wako, wakazi wa Siyoni shangilieni kwa sababu ya Mfalme wenu. Lisifuni jina lake kwa ngoma, mwimbieni kwa ngoma na zeze.