Mfalme wa Ashuru akawatuma jemadari wake, na mkuu wa matowashi, na kamanda wake, toka Lakishi, kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu, pamoja na jeshi kubwa. Nao wakakwea wakafika Yerusalemu. Na walipokwisha kufika, wakaja wakasimama karibu na mfereji wa birika la juu, lililo katika njia kuu ya kuuendea Uwanda wa Dobi.
Basi mambo yote ya Hezekia yaliyosalia, na ushujaa wake wote, tena alivyolifanya birika na mfereji, akaleta maji ndani ya mji, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda?
Naye huyo Hezekia ndiye aliyezuia chemchemi ya juu ya maji ya Gihoni, akayaleta chini moja kwa moja upande wa magharibi wa mji wa Daudi. Akafanikiwa Hezekia katika kazi zake zote.
na kwa lango la chemchemi, wakienda moja kwa moja mbele yao, wakapanda madaraja ya mji wa Daudi, uinukapo ukuta, juu ya nyumba ya Daudi, mpaka lango la maji upande wa mashariki.
Na lango la chemchemi akalijenga Shalumu, mwana wa Kolhoze, mkuu wa Mispa akalitengeneza lango la Chemchemi akalijenga na kulifunika, akasimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake, na huo ukuu wa birika la Shiloa karibu na bustani ya mfalme, mpaka madaraja yashukayo kutoka mji wa Daudi.
Baada yake akajenga Nehemia, mwana wa Azbuki, mkuu wa nusu ya mtaa wa Beth-suri, mpaka mahali paelekeapo makaburi ya Daudi, na mpaka birika lililofanyizwa, na mpaka nyumba ya wapiganaji.