Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza; na barua zikaandikwa, kama vile Hamani alivyoagiza, kwa wakuu wa mfalme, na wakuu wa mikoa, na wakuu wa kila taifa; kila mkoa kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; zikaandikwa kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutiwa mhuri kwa pete yake.
Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na wakuu wa tarafa na wakuu wa mikoa kuanzia Bara Hindi mpaka Kushi, mikoa mia moja na ishirini na saba, kila mkoa kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao.
Hata ulipofika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku yake ya kumi na tatu, amri ya mfalme na mbiu yake ilipowadia kutekelezwa; ambayo siku ile adui za Wayahudi walitumaini kuwatawala, bali kumebadilika kinyume, hata Wayahudi waliwatawala wale waliowachukia;
Lakini Wayahudi wa Susa walikusanyika siku ya kumi na tatu ya mwezi huo, na siku ya kumi na nne pia; na siku ya kumi na tano ya mwezi uo huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha.