Isaya 4 - Swahili Revised Union Version1 Na siku hiyo wanawake saba watamshika mwanaume mmoja wakisema, Tutakula chakula chetu, na kuvaa nguo zetu wenyewe, lakini tuitwe tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetu. Utukufu wa siku za usoni kwa mabaki wa Sayuni 2 Siku hiyo chipukizi la BWANA litakuwa zuri, lenye utukufu, na matunda ya nchi yatakuwa mema sana, na kupendeza, kwa ajili ya Waisraeli wale waliookoka. 3 Tena itakuwa ya kwamba yeye aliyebaki katika Sayuni, na yeye aliyeachwa ndani ya Yerusalemu, ataitwa mtakatifu; yaani, kila mmoja aliyeandikwa miongoni mwa hao walio hai ndani ya Yerusalemu; 4 hapo Bwana atakapokuwa ameuosha uchafu wa hao binti za Sayuni na kuisafisha damu ya Yerusalemu kati yake, kwa roho ya hukumu na kwa roho ya kuteketeza. 5 Tena juu ya makao yote ya mlima Sayuni, na juu ya makusanyiko yake, BWANA ataumba wingu na moshi wakati wa mchana, na mwangaza wa miali ya moto wakati wa usiku; kwa maana juu ya utukufu wote itatandazwa sitara. 6 Kisha kutakuwa na hema kuwa uvuli wakati wa mchana kwa sababu ya joto, na kuwa mahali pa kukimbilia na kujificha wakati wa tufani na mvua. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya