Hosea 11 - Swahili Revised Union VersionHuruma za Mungu kwa Israeli 1 Israeli alipokuwa mtoto, nilikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri. 2 Kadiri walivyowaita ndivyo walivyoondoka na kuwaacha; waliwatolea dhabihu Mabaali, na kuzifukizia uvumba sanamu za kuchonga. 3 Lakini nilimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; niliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa niliwaponya. 4 Niliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nilikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandaa chakula mbele yao. 5 Hatarudi tena nchi ya Misri; bali huyo Mwashuri atakuwa mfalme wake; kwa sababu walikataa kurejea. 6 Na upanga utaiangukia miji yake, utayaharibu makomeo yake na kuyala, kwa sababu ya mashauri yao wenyewe. 7 Na watu wangu wamejipinda kuniacha; ingawa wawaita kwenda kwake Aliye Juu, hapana hata mmoja atakayemtukuza. 8 Niwezeje kukuacha, Efraimu? Niwezeje kukuachilia Israeli? Niwezeje kukufanya kama Adma? Niwezeje kukuweka kama Seboimu? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja. 9 Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitamwangamiza Efraimu tena; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji. 10 Watakwenda kumfuata BWANA, atakayenguruma kama simba; kwa maana atanguruma, nao watoto watakuja kutoka magharibi wakitetemeka. 11 Watakuja wakitetemeka kama shomoro, toka Misri, na kama hua, toka nchi ya Ashuru; nami nitawakalisha katika nyumba zao, asema BWANA. 12 Efraimu amenizunguka kwa maneno ya uongo, na nyumba ya Israeli kwa udanganyifu; na Yuda hata sasa anasitasita kwa Mungu, na kwake aliye Mtakatifu, naye ni mwaminifu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya