Zekaria 13 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC1 Katika siku hiyo watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, watafunguliwa chemchemi ya kuwatakasa kutoka kwa dhambi na kwa unajisi. Kuabudu sanamu kwakatiliwa mbali 2 Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema BWANA wa majeshi, nitakatilia mbali majina ya sanamu katika nchi, yasikumbukwe tena; pia nitawafukuza manabii, na roho ya uchafu, watoke katika nchi. 3 Tena itakuwa ya kwamba, mtu awaye yote atakapotoa unabii, basi baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, Hutaishi; kwa maana unanena maneno ya uongo kwa jina la BWANA; na baba yake na mama yake waliomzaa watamtumbua atoapo unabii. 4 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; wala hawatavaa joho la nywele ili kudanganya watu; 5 bali atasema, Mimi si nabii kamwe; mimi ni mkulima wa nchi; kwa maana nilifanywa mtumwa tokea ujana wangu. 6 Na mtu yeyote akimwuliza, Je! Majeraha haya yote uliyo nayo katikati ya mikono yako ni nini? Naye atajibu, Ni majeraha niliyotiwa katika nyumba ya rafiki zangu. Mchungaji apigwa na kundi kutawanywa 7 Amka, Ee upanga, juu ya mchungaji wangu, na juu ya mtu aliye mwenzangu, asema BWANA wa majeshi; mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika; nami nitaugeuza mkono wangu juu ya wadogo. 8 Hata itakuwa, ya kwamba katika nchi yote mafungu mawili yatakatiliwa mbali, nao watakufa, asema BWANA; lakini fungu la tatu litabaki humo. 9 Nami nitalileta fungu lile la tatu na kulipitisha kati ya moto, nami nitawasafisha kama fedha isafishwavyo, nami nitawajaribu kama dhahabu ijaribiwavyo; wataliitia jina langu, nami nitawasikia; mimi nitasema, Watu hawa ndio wangu; nao watasema, BWANA ndiye Mungu wangu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya