Zaburi 98 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSifa kwa mwamuzi wa Dunia Zaburi. 1 Mwimbieni BWANA wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kulia, Na mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. 2 BWANA ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake. 3 Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu. 4 Mshangilieni BWANA, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni sifa. 5 Mwimbieni BWANA sifa kwa kinubi, Kwa kinubi na sauti tamu. 6 Kwa panda na sauti ya baragumu. Shangilieni mbele za Mfalme, BWANA. 7 Bahari na ivume na vyote viijazavyo, Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake. 8 Mito na ipige makofi, Milima na iimbe pamoja kwa furaha. 9 Mbele za BWANA; Kwa maana anakuja kuihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa uaminifu, Na mataifa kwa adili. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya