Zaburi 90 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCKITABU CHA NNE Mungu adumuye milele na binadamu apitaye Sala ya Musa, Mtu wa Mungu. 1 Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, Kizazi baada ya kizazi. 2 Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu. 3 Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu. 4 Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku. 5 Wawafutilia wanadamu mbali kama ndoto, wao ni kama majani yameayo asubuhi. 6 Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka. 7 Maana tumeangamia kwa hasira yako, Na kwa ghadhabu yako tumezidiwa. 8 Umeyaweka maovu yetu mbele zako, Dhambi zetu za siri katika mwanga wa uso wako. 9 Maana kwa hasira yako maisha yetu yanapita punde, Maisha yetu yanaisha kama kite. 10 Miaka ya maisha yetu ni sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Tena kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana wakati unapita upesi nasi kutokomea punde. 11 Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako inayolingana na kicho chako? 12 Basi, utufundishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima. 13 Urudi, Ee BWANA utakasirika hadi lini? Wahurumie watumishi wako. 14 Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote. 15 Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa, Miaka sawa na ile tuliyopatwa na maovu. 16 Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, Na utukufu wako kwa watoto wao. 17 Na fadhili za BWANA, Mungu wetu, ziwe juu yetu, Na kazi ya mikono yetu uifanye thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uifanikishe. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya