Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Zaburi 89 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Agano la Mungu wa Daudi Utenzi wa Ethani Mwezrahi.

1 Fadhili za BWANA nitaziimba milele; Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.

2 Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele; Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.

3 Nimefanya agano na mteule wangu, Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.

4 Wazao wako nitawaimarisha milele, Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele.

5 Ee BWANA, mbingu zitayasifu maajabu yako, Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu.

6 Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na BWANA? Ni nani afananaye na BWANA miongoni mwa malaika?

7 Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka.

8 BWANA, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka.

9 Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo, wewe unayatuliza.

10 Ndiwe uliyemponda Rahabu akawa kama aliyeuawa, Kwa mkono hodari umewatawanya wakuchukiao.

11 Mbingu ni mali yako, nchi nayo ni mali yako, Ulimwengu na vyote viujazavyo Ndiwe uliyeupiga msingi wake.

12 Kaskazini na kusini ndiwe uliyeziumba, Tabori na Hermoni hulifurahia jina lako.

13 Mkono wako ni mkono wenye uweza, Mkono wako una nguvu, Mkono wako wa kulia umetukuka.

14 Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako, Fadhili na kweli zimo mbele za uso wako.

15 Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe, Ee BWANA, waendao, katika nuru ya uso wako.

16 Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa, Na kwa haki yako hutukuzwa.

17 Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe, Na kwa radhi yako pembe yetu itatukuka.

18 Maana ngao yetu ni BWANA, Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli.

19 Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa maono, Ukasema, Nimempa aliye hodari msaada; Nimemtukuza aliyechaguliwa miongoni mwa watu.

20 Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, Nimempaka mafuta yangu matakatifu.

21 Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu.

22 Adui hatamwonea, Wala mwana wa uovu hatamtesa.

23 Bali nitawaponda watesi wake mbele yake, Nitawapiga wanaomchukia.

24 Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo, Na kwa jina langu pembe yake itatukuka.

25 Nitaweka mkono wake juu ya bahari, Na mkono wake wa kulia juu ya mito.

26 Yeye ataniita, Wewe ni baba yangu, Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.

27 Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wote wa dunia.

28 Hata milele nitamwekea fadhili zangu, Na agano langu naye litadumu hata milele.

29 Wazao wake nao nitawadumisha milele, Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu.

30 Wanawe wakiiacha sheria yangu, Wasiende katika hukumu zangu,

31 Wakizivunja amri zangu, Wasiyashike maagizo yangu,

32 Basi, nitawarudi makosa yao kwa fimbo, Na uovu wao kwa mapigo.

33 Lakini fadhili zangu sitamwondolea yeye, Wala sitafanya uaminifu wangu kuwa uongo.

34 Mimi sitalivunja agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.

35 Neno moja nimeliapa kwa utakatifu wangu, Hakika sitamwambia Daudi uongo,

36 Wazawa wake watadumu milele, Na kiti chake cha enzi kuwa mbele yangu kama jua.

37 Kitathibitika milele kama mwezi; Shahidi mwaminifu aliye mbinguni.

38 Lakini wewe umemtupa na kumkataa, Umemghadhibikia masihi wako.

39 Umechukizwa na agano la mtumishi wako, Umelinajisi taji lake na kulitupa chini.

40 Umeyabomoa maboma yake yote, Umezifanya ngome zake kuwa magofu.

41 Wote wapitao njiani wanateka mali zake; Amedharauliwa na jirani zake;

42 Umeutukuza mkono wa kulia wa watesi wake; Umewafurahisha wote wanaomchukia.

43 Pia umeurudisha nyuma ukali wa upanga wake; Wala hukumsimamisha vitani.

44 Umeikomesha fahari yake; Kiti chake cha enzi umekitupa chini.

45 Umezipunguza siku za ujana wake; Umemvika aibu.

46 Hadi lini, Ee BWANA? Utajificha hata milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto hadi lini?

47 Ukumbuke jinsi mimi nisivyo wa kudumu; Kwa ubatili gani umeiumba jamii ya wanadamu!

48 Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti, Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu?

49 Bwana, ziko wapi fadhili zako za kwanza, Ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako?

50 Ukumbuke, Ee Bwana, Wanavyosimangwa watumishi wako; Jinsi ninavyostahimili kifuani mwangu Masimango ya watu wengi.

51 Ambayo adui zako wamesimanga, Ee BWANA, Naam, wamezisimanga hatua za masihi wako.


* * *

52 Na ahimidiwe BWANA milele. Amina na Amina.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo