Zaburi 84 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCShangwe ya kuabudu katika hekalu Kwa mwimbishaji: kwa mtindo wa Gitithi. Ya Wakorahi. Zaburi. 1 Maskani zako zapendeza kama nini, Ee BWANA wa majeshi! 2 Nafsi yangu imezionea shauku nyua za BWANA, Naam, na kuzikondea. Moyo wangu na mwili wangu Vinamlilia Mungu aliye hai. 3 Hata Shomoro ameona nyumba, Na mbayuwayu amejipatia kiota, Alipoweka makinda yake, Kwenye madhabahu zako, Ee BWANA wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu. 4 Heri wakaao nyumbani mwako, Wanakuhimidi daima. 5 Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako, Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake. 6 Wapitapo katika bonde la baraka, Hulifanya kuwa chemchemi, Naam, mvua ya vuli hulijaza baraka. 7 Huendelea toka nguvu hata nguvu, Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu. 8 BWANA, Mungu wa majeshi, uyasikie maombi yangu, Ee Mungu wa Yakobo, usikilize, wako. 9 Ee Mungu, ngao yetu, uangalie, Umtazame uso masihi 10 Hakika siku moja katika nyua zako Ni bora kuliko siku elfu kwingineko; Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu, Kuliko kuishi katika hema za uovu. 11 Kwa kuwa BWANA, Mungu, ni jua na ngao, BWANA atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu. 12 Ee BWANA wa majeshi, Heri mwanadamu anayekutumaini Wewe. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya