Zaburi 83 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSala ya hukumu juu ya adui wa Israeli Wimbo. Zaburi ya Asafu. 1 Ee Mungu, usistarehe, Ee Mungu, usinyamae, wala usitulie. 2 Maana adui zako wanafanya ghasia, Nao wakuchukiao wameviinua vichwa vyao. 3 Juu ya watu wako wanafanya hila, Na kushauriana juu yao uliowaficha. 4 Wamesema, Njoni, tuwakatilie mbali wasiwe taifa, Na jina la Israeli halitakumbukwa tena. 5 Maana wanashauriana kwa moyo mmoja, Juu yako wanafanyana agano. 6 Hema za Edomu, na Waishmaeli, Na Moabu, na Wahagari, 7 Gebali, na Amoni, na Amaleki, Na Filisti, nao wanaokaa Tiro, 8 Ashuri naye amepatana nao, Wamewasaidia wana wa Lutu. 9 Uwatende kama ulivyowatenda Midiani, Sisera, Na Yabini, penye kijito cha Kishoni. 10 Ambao waliangamizwa Endori; Wakawa samadi juu ya nchi. 11 Uwafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu, Na wakuu wao wote kama Zeba na Zalmuna. 12 Ambao Walisema, Na tutamalaki makao ya Mungu. 13 Ee Mungu, uwafanye kama mavumbi ya kisulisuli, Kama ya makapi mbele ya upepo, 14 Kama moto uteketezao msitu, Kama miali ya moto iiwashayo milima, 15 Ndivyo utakavyowafuatia kwa tufani yako, Na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako. 16 Uzijaze nyuso zao fedheha; Ili wapate kulitafuta jina lako, Ee BWANA. 17 Waaibike, wafadhaike milele, Naam, watahayarike na kupotea. 18 Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye Juu, juu ya nchi yote. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya