Zaburi 72 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSala ya kumtakia mfalme neema Ya Sulemani 1 Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako, Na mwana wa mfalme haki yako. 2 Atawaamua watu wako kwa haki, Na watu wako walioonewa kwa hukumu. 3 Milimana iwaletee watu amani, Na pamoja na vilima, ilete haki. 4 Na atawatetea watu walioonewa, Awaokoe wahitaji, na kumwaangamiza mdhalimu. 5 Watakuogopa wakati wote wa kudumu jua, Na wakati wa kung'aa mwezi kizazi hata kizazi. 6 Atashuka kama mvua juu ya majani yaliyokatwa, Kama manyunyu yainyweshayo nchi. 7 Haki na isitawi wakati wa maisha yake yote, Nayo amani iwepo, hadi mwezi utakapokoma. 8 Na awe na enzi toka bahari hadi bahari, Toka Mto hadi miisho ya dunia. 9 Wakaao jangwani na wainame mbele zake; Adui zake na warambe mavumbi. 10 Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi; Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa. 11 Naam, wafalme wote na wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie. 12 Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo, Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. 13 Atawahurumia wanyonge na maskini, Na nafsi za wahitaji ataziokoa. 14 Atawakomboa kutoka kwa maonevu na udhalimu, Maana damu yao ina thamani machoni pake. 15 Na aishi maisha marefu! Na wampe dhahabu ya Sheba; Na wamwombee daima; Na kumbariki mchana kutwa. 16 Na uwepo wingi wa nafaka Katika ardhi juu ya milima; Matunda yake na yawayewaye kama ilivyo katika milima ya Lebanoni, Na watu wa mjini wasitawi kama majani ya nchi. 17 Jina lake na lidumu milele, Pindi ling'aapo jua, umaarufu wake uwepo; Mataifa yote na wabarikiwe katika yeye, Na kumwita heri. * * * 18 Na ahimidiwe BWANA, Mungu, Mungu wa Israeli, Atendaye miujiza Yeye peke yake; 19 Jina lake tukufu na lihimidiwe milele; Dunia yote na ijae utukufu wake. Amina na Amina. * * * 20 Maombi ya Daudi mwana wa Yese, yamekwisha. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya