Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Zaburi 68 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Sifa na shukrani Kwa mwimbishaji. Ya Daudi. Zaburi. Wimbo.

1 Mungu na ainuke, adui zake watawanyike, Nao wamchukiao huukimbia uso wake.

2 Kama moshi upeperushwavyo, Ndivyo uwapeperushavyo wao; Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto, Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu.

3 Bali wenye haki hufurahi, Na kuushangilia uso wa Mungu, Naam, hupiga kelele kwa furaha.

4 Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mwimbieni wimbo yeye apitaye katika mawingu, Jina lake ni YAHU; Shangilieni mbele zake.

5 Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Ni Mungu aliye katika kao lake takatifu.

6 Mungu huwapa wapweke makao yao; Huwapa wafungwa uhuru na kuwafanikisha; Bali wakaidi huishi katika nchi kavu.

7 Ee Mungu, ulipowaongoza watu wako, Ulipopita nyikani,

8 Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli.

9 Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu.

10 Watu wako wakafanya makao ya huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.

11 Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa;

12 Wafalme wa majeshi wanakimbia, wanakimbia; Na mwanamke akaaye nyumbani anagawa nyara.

13 Kwa nini kulala mazizini arukapo hua, Mbawa zake ziking'aa kama fedha Na manyoya yake kama dhahabu?

14 Mwenyezi Mungu alipotawanya wafalme huko, Kulinyesha theluji katika Salmoni.

15 Ni mlima wa Mungu mlima Bashani, Ni mlima mrefu mlima Bashani.

16 Enyi milima mirefu, kwani kuutazama kwa wivu Mlima alioutamani Mungu akae juu yake? Naam, BWANA atakaa juu yake milele.

17 Magari ya Mungu ni elfu ishirini, maelfu kwa maelfu; Bwana yumo kati yao kama katika Sinai, Katika patakatifu.

18 Wewe umepaa juu, umeteka mateka, Umepewa vipawa katikati ya wanadamu; Naam, hata na wakaidi, BWANA Mungu akae nao.

19 Na ahimidiwe Bwana, Siku kwa siku hutuchukulia mzigo wetu; Mungu ndiye wokovu wetu.

20 Mungu wetu ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.

21 Naam, Mungu atakipasua kichwa cha adui zake, Utosi wenye nywele wa mtu afululizaye kukosa.

22 Bwana alisema, Kutoka Bashani nitawarudisha, Nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari;

23 Uuchovye mguu wako katika damu ya adui zako, Na ulimi wa mbwa zako upate sehemu yake.

24 Ee Mungu, wameiona miendo yako; Miendo ya Mungu wangu, Mfalme wangu, katika patakatifu.

25 Waimbaji hutangulia, nyuma yao wapigao vinanda, Kati ya wanawali wapiga matari.

26 Mhimidini Mungu katika mikutano, Bwana katika makusanyiko ya Israeli.

27 Yuko Benyamini mdogo, mtawala wao; Wakuu wa Yuda, kundi lao; Wakuu wa Zabuloni; Wakuu wa Naftali.

28 Ee Mungu, uziamuru nguvu zako; Ee Mungu, uwe hodari uliyetufanyia makuu.

29 Kwa ajili ya hekalu lako Yerusalemu Wafalme watakuletea hedaya.

30 Mkemee mnyama wa mafunjoni; Kundi la mafahali, na ndama za watu; Hata wanyenyekee na kuleta vipande vya fedha, Uwatawanye watu wapendao vita.

31 Masheki watakuja kutoka Misri, Kushi itahimiza kumnyoshea Mungu mikono yake.

32 Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu, Msifuni Bwana kwa nyimbo.

33 Apandaye mbingu za mbingu za tangu milele; Aitoa sauti yake, sauti ya nguvu.

34 Mhesabieni Mungu nguvu; Enzi yake imo juu ya Israeli; Na nguvu zake ziko mawinguni.

35 Mungu ni mwenye kutisha Kutoka patakatifu pako. Ndiye Mungu wa Israeli; Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo. Na ahimidiwe Mungu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo