Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Zaburi 66 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Sifa kwa ajili ya wema wa Mungu kwa Israeli Kwa mwimbishaji. Wimbo. Zaburi.

1 Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,

2 Imbeni utukufu wa jina lake, Tukuzeni sifa zake.

3 Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini! Kwa ajili ya wingi wa nguvu zako, Adui zako watakuja kunyenyekea mbele zako.

4 Nchi yote itakusujudia na kukuimbia, Naam, italiimbia jina lako.

5 Njoni myaone matendo ya Mungu; Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu;

6 Aligeuza bahari ikawa nchi kavu; Katika mto walivuka kwa miguu; Huko ndiko tulikomfurahia yeye.

7 Atawalaye kwa uweza wake milele; Ambaye macho yake yanaangalia mataifa; Hebu wanaoasi wasijitukuze nafsi zao.

8 Enyi mataifa, mtukuzeni Mungu wetu, Itangazeni sauti ya sifa zake;

9 Aliyeiweka nafsi yetu katika uhai, Wala hakuuacha mguu wetu usogezwe.

10 Kwa maana umetupima, Ee Mungu, Umetujaribu inavyojaribiwa fedha.

11 Ulituingiza ndani ya wavu, Na kuweka viunoni mwetu mzigo uliotulemea.

12 Uliwapandisha watu Juu ya vichwa vyetu. Tulipitia motoni na majini; Ukatutoa na kutuleta kwenye ufanisi.

13 Nitaingia nyumbani mwako na kafara; Nitaondoa kwako nadhiri zangu;

14 Ambazo midomo yangu ilizinena; Kinywa changu kikazisema nilipokuwa taabuni.

15 Kafara za vinono nitakutolea, Pamoja na fukizo la kondoo dume, Nitatoa ng'ombe pamoja na mbuzi.

16 Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu, Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.

17 Nilimwita kwa kinywa changu, Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi wangu.

18 Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana asingesikia.

19 Hakika Mungu amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu.

20 Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo