Zaburi 6 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSala ya kuponywa ugonjwa hatari Kwa mwimbishaji: kwa ala za muziki zenye nyuzi; kulingana na mtindo wa Sheminithi. Zaburi ya Daudi. 1 BWANA, usinikemee kwa hasira yako, Wala usinirudi kwa ghadhabu yako. 2 BWANA, unifadhili, maana ninanyauka; BWANA, uniponye, mifupa yangu imefadhaika. 3 Na nafsi yangu imefadhaika sana; Na Wewe, BWANA, hadi lini? 4 BWANA urudi, uniopoe nafsi yangu, Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. 5 Maana mautini hapana kumbukumbu lako; Katika kuzimu ni nani atakayekushukuru? 6 Nimechoka kwa kuugua kwangu; Kila usiku nakibubujikia kitanda changu; Nililowesha godoro langu kwa machozi yangu. 7 Macho yangu yameharibika kwa masumbufu, Na kuchakaa kwa sababu yao wanaoniudhi. 8 Ondokeni kwangu, ninyi nyote mtendao uovu; Kwa kuwa BWANA ameisikia sauti ya kilio changu. 9 BWANA ameisikia dua yangu; BWANA atayatakabali maombi yangu. 10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafla wataaibika. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya