Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Zaburi 44 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Kilio cha kitaifa na sala kwa ajili ya msaada Kwa mwimbishaji. Funzo la Wakorahi.

1 Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu Baba zetu wametuambia, Matendo uliyoyatenda siku zao, siku za kale.

2 Wewe kwa mkono wako uliwafukuza mataifa, Ukawakalisha wao. Wewe uliwatesa watu wa nchi, Ukawafanikisha wao.

3 Maana hawakuitwaa nchi kwa upanga wao, Wala hawakupata ushindi kwa mkono wao; Bali mkono wako wa kulia, naam, mkono wako, Na nuru ya uso wako, kwa kuwa ulipendezwa nao.

4 Ee Mungu, Wewe ndiwe mfalme wangu, Uagize mambo ya wokovu kwa Yakobo.

5 Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu; Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao.

6 Maana sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hauwezi kuniokoa.

7 Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa kutoka kwa watesi wetu; Na watuchukiao umewaaibisha.

8 Tumejisifia Mungu mchana kutwa, Na jina lako tutalishukuru milele.

9 Lakini umetutupa, umetufedhehesha, Wala huendi na majeshi yetu.

10 Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo, Na watuchukiao wanajipatia mateka.

11 Umetutoa kama kondoo tuwe chakula, Na kututawanya kati ya mataifa.

12 Wawauza watu wako bila kupata mali, Wala hukupata faida kwa thamani yao.

13 Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.

14 Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa, Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi.

15 Mchana kutwa fedheha yangu i mbele yangu, Na aibu imeufunika uso wangu,

16 Kwa sauti ya mwenye kulaumu na kukufuru, Kwa sababu ya adui na mjilipiza kisasi.

17 Haya yote yametupata, bali hatukukusahau, Wala hatukulivunja agano lako.

18 Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma, Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako,

19 Japo ulituponda katika pango la mbwamwitu, Na kutufunika kwa uvuli wa mauti.

20 Ikiwa tumelisahau jina la Mungu wetu, Au kumnyoshea mungu mgeni mikono yetu;

21 Je! Mungu hangegundua jambo hilo? Maana ndiye azijuaye siri za moyo.

22 Hasha! Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; Tunafanywa kama kondoo waendao kuchinjwa.

23 Amka, Bwana, mbona umelala? Ondoka, usitutupe milele.

24 Mbona unatuficha uso wako, Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu?

25 Maana nafsi yetu imeinama mavumbini, Tumbo letu limegandamana na nchi.

26 Uinuke, uwe msaada wetu, Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo