Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Zaburi 40 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Shukrani kwa kuponywa na sala ya kutaka msaada Kwa mwimbishaji. Ya Daudi. Zaburi.

1 Nilimngoja BWANA kwa subira, Akaniinamia na kusikia kilio changu.

2 Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu.

3 Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumainia BWANA.

4 Heri aliyemfanya BWANA kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo.

5 Ee BWANA, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki.

6 Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Umetuzidishia ila masikio, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.

7 Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la kitabu nimeandikiwa,)

8 Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.

9 Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa. Sikuizuia midomo yangu; Ee BWANA, unajua.

10 Sikusitiri haki yako moyoni mwangu; Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha fadhili zako wala kweli yako Katika kusanyiko kubwa.

11 Nawe, BWANA, usinizuilie rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima.

12 Kwa maana mabaya yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona. Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu, Nami nimevunjika moyo.

13 Ee BWANA, uwe radhi kuniokoa, Ee BWANA, unisaidie hima.

14 Waaibike na wafedheheke, Wote wanaotaka kuniua. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu.

15 Wafadhaike kwa aibu yao, Wanaoniambia Ewe! Ewe!

16 Washangilie na wakufurahie, Wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako Waseme daima, BWANA ni Mkuu.

17 Nami ni maskini na mhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Mungu wangu, usikawie.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo