Zaburi 34 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSifa kwa kukombolewa katika shida Ya Daudi, alipojifanya mwenye kichaa mbele za Abimeleki, ndipo akafukuzwa na kumtoroka. 1 Nitamhimidi BWANA kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima. 2 Katika BWANA nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie na kufurahi. 3 Mtukuzeni BWANA pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja. 4 Nilimtafuta BWANA, naye akanijibu, Akaniokoa kutoka kwa hofu zangu zote. 5 Mwelekezeeni macho, mpate kufurahi, Na nyuso zenu hazitaaibishwa kamwe. 6 Maskini huyu aliita, BWANA akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote. 7 Malaika wa BWANA huwazungukia, Wamchao na kuwaokoa. 8 Onjeni muone ya kuwa BWANA yu mwema; Heri mtu yule anayemtumainia. 9 Mcheni BWANA, enyi watakatifu wake, Maana, wamchao hawapungukiwi kitu. 10 Wanasimba hutindikiwa, na kuona njaa; Bali wamtafutao BWANA hawapungukiwi kitu chochote kilicho chema. 11 Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha BWANA. 12 Ni nani atamaniye uzima na atakaye kuishi, Siku nyingi afurahie mema? 13 Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila. 14 Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. 15 Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. 16 Uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. 17 Walilia, naye BWANA akasikia, Akawaponya kutoka kwa taabu zao zote. 18 BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo, Na huwaokoa waliopondeka roho. 19 Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini BWANA kutoka kwayo yote. 20 Huihifadhi mifupa yake yote, Usivunjike hata mmoja. 21 Uovu utamwua asiye haki, Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa. 22 BWANA huzikomboa nafsi za watumishi wake, Wote wamkimbiliao hawatahukumiwa. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya