Zaburi 21 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCShukrani kwa ushindi Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. 1 Ee BWANA, mfalme atazifurahia nguvu zako, Na wokovu wako ataufanyia shangwe nyingi sana. 2 Umempa haja ya moyo wake, Wala hukumzuilia matakwa ya midomo yake. 3 Maana umemsogezea baraka za heri, Umemvika taji la dhahabu safi kichwani pake. 4 Alikuomba uhai, ukampa, Muda mrefu wa siku nyingi, milele na milele. 5 Utukufu wake ni mkuu kwa wokovu wako, Heshima na adhama waweka juu yake. 6 Maana umemfanya kuwa baraka za milele, Wamfurahisha kwa furaha ya uso wako. 7 Kwa kuwa mfalme humtumainia BWANA, Na kwa fadhili zake Aliye Juu hatatikisika. 8 Mkono wako utawapata adui zako wote, Mkono wako wa kulia utawapata wanaokuchukia. 9 Utawafanya kuwa kama tanuri ya moto, Wakati wa ghadhabu yako. BWANA atawameza kwa ghadhabu yake, Na moto utawateketeza. 10 Matunda yao utayaharibu na kuyaondoa katika nchi, Na wazao wao katika wanadamu. 11 Wakipanga kukutenda mabaya, Kwa miango ya hila, hawatafanikiwa. 12 Kwa maana utawatimua utawafanya wakimbie, Kwa upote wa uta wako utazilenga nyuso zao. 13 Ee BWANA, utukuzwe kwa nguvu zako, Nasi tutaimba na kuuhimidi uwezo wako. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya