Zaburi 20 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSala ya ushindi Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. 1 BWANA akujibu siku ya dhiki, Jina la Mungu wa Yakobo likuinue. 2 Akutumie msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni. 3 Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. 4 Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kukutimizia mipango yako yote. 5 Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu. BWANA akutimizie matakwa yako yote. 6 Sasa najua kuwa BWANA amwokoa masihi wake; Atamjibu toka mbingu zake takatifu, Kwa matendo makuu ya wokovu Ya mkono wake wa kulia. 7 Hawa wanataja magari na hawa farasi, Lakini sisi tutalitaja jina la BWANA, Mungu wetu. 8 Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama. 9 BWANA, umwokoe mfalme, Utuitikie siku tuitayo. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya