Zaburi 2 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCAhadi ya Mungu kwa mtiwa mafuta wake 1 Mbona mataifa yanafanya ghasia, Na watu kuwaza mambo ya bure? 2 Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya BWANA, Na juu ya masihi wake, 3 Na tuvipasue vifungo vyao, Na kuzitupa mbali nasi kamba zao. 4 Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana anawafanyia dhihaka. 5 Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake, Na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake, akisema: 6 Nami nimemweka mfalme wangu Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu. 7 Nitaihubiri amri; BWANA aliniambia, Wewe ni mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. 8 Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako. 9 Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. 10 Na sasa, enyi wafalme, iweni na hekima, Enyi watawala wa dunia, mwaonywa. 11 Mtumikieni BWANA kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka. 12 Shikeni yaliyo bora, asije akafanya hasira Nanyi mkapotea njiani, Kwa kuwa hasira yake huwaka upesi; Heri wote wanaomkimbilia. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya