Zaburi 18 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCShukrani za kifalme kwa ushindi Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa BWANA, aliyomwambia BWANA wakati BWANA alipomwokoa kutoka kwa mkono wa adui zake wote na kutoka kwa mkono wa Sauli. Akasema: 1 Wewe, BWANA, nguvu yangu, nakupenda sana; 2 BWANA ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu. 3 Namwita BWANA astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu. 4 Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. 5 Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. 6 Katika shida yangu nilimwita BWANA, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake. 7 Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikatingizika; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu. 8 Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto wa kuteketeza ukatoka kinywani mwake, Makaa ya moto yakamtoka. 9 Aliziinamisha mbingu akashuka, Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake. 10 Akapanda juu ya kerubi akaruka, Naam, aliruka upesi juu ya mabawa ya upepo. 11 Alifanya giza kuwa mahali pake pa kujificha, Kuwa hema yake ya kumzunguka. Akiwa katika giza la mawingu mazito yaliyojaa maji. 12 Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Kukapita mawingu yake makuu. Ikashuka mvua ya mawe na makaa ya moto. 13 BWANA alinguruma kutoka mbinguni, Yeye Aliye Juu akaitoa sauti yake, Mvua ya mawe na makaa ya moto. 14 Akaipiga mishale yake akawatawanya, Naam, umeme mwingi sana, akawatapanya. 15 Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee BWANA, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako. 16 Alinishukia kutoka juu, akanichukua, Na kunitoa katika maji mengi. 17 Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia, Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi. 18 Walinikabili siku ya msiba wangu, Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu. 19 Akanitoa akanipeleka panapo nafasi, Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami. 20 BWANA alinitendea sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa. 21 Maana nimezishika njia za BWANA, Wala sikumwasi Mungu wangu. 22 Hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu, Wala amri zake sikubandukana nazo. 23 Nami nilikuwa mkamilifu mbele zake, Nikajilinda na uovu wangu. 24 Ndipo BWANA akanilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake. 25 Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili; Kwa mkamilifu utajionesha kuwa mkamilifu; 26 Kwake ajitakasaye utajionesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionesha kuwa mkaidi. 27 Maana Wewe wawaokoa watu wanaoonewa, Na macho ya kiburi utayadhili. 28 Kwa kuwa Wewe unaiwasha taa yangu; BWANA Mungu wangu aniangazia giza langu. 29 Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi, Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta. 30 Mungu, njia yake ni kamilifu, Ahadi ya BWANA imehakikishwa, Yeye ndiye ngao yao. Wote wanaomkimbilia. 31 Maana ni nani aliye Mungu ila BWANA? Ni nani aliye mwamba ila Mungu wetu? 32 Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu. 33 Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu, Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. 34 Anaifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba. 35 Nawe umenipa ngao ya wokovu wako, Mkono wako wa kulia umenitegemeza, Na unyenyekevu wako umenikuza. 36 Umezipanulia nafasi hatua zangu, Na miguu yangu haikuteleza. 37 Nitawafuatia adui zangu na kuwapata, Wala sitarudi nyuma hadi wakomeshwe. 38 Nitawapigapiga wasiweze kusimama, Wataanguka chini ya miguu yangu. 39 Nawe umenipa nguvu za vita, Hunitiishia chini yangu walionishambulia. 40 Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Nao walionichukia nimewakatilia mbali. 41 Walipiga yowe, lakini hakuna wa kuokoa, Walimwita BWANA lakini hakuwajibu, 42 Nikawaponda kama mavumbi mbele ya upepo, Nikawatupa nje kama matope ya njiani. 43 Umeniokoa kutoka kwa mashindano ya watu, Umenifanya niwe kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. 44 Mara tu waliposikia habari zangu, wakanitii. Wageni walinijia wakinyenyekea. 45 Wageni nao walitepetea, Walitoka katika ngome zao wakitetemeka. 46 BWANA ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu; 47 Ndiye Mungu anilipizaye kisasi; Na kuwatiisha watu chini yangu. 48 Huniponya na adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia, Na kuniponya na mtu mjeuri. 49 Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. 50 Ampa mfalme wake wokovu mkuu, Amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na wazawa wake hata milele. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya