Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Zaburi 145 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Ukuu na wema wa Mungu Sifa. Ya Daudi.

1 Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, Nitalihimidi jina lako milele na milele.

2 Kila siku nitakuhimidi, Nitalisifu jina lako milele na milele.

3 BWANA ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana, Wala ukuu wake hauchunguziki.

4 Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako, Kitayatangaza matendo yako makuu.

5 Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako, Na matendo yako yote ya ajabu.

6 Watu watayataja matendo yako ya kutisha, Nami nitausimulia ukuu wako.

7 Watasimulia juu ya ukuu wa wema wako mwingi. Na wataiimba haki yako kwa sauti.

8 BWANA ni mwenye fadhili na huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,

9 BWANA ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake ziko juu ya vyote alivyoumba.

10 Ee BWANA, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi.

11 Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kusena uweza wako.

12 Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.

13 Ufalme wako ni ufalme wa milele, BWANA ni mwaminifu katika maneno yake yote, Na mwenye fadhili katika matendo yake yote Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.

14 BWANA huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini.

15 Macho ya watu wote yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake.

16 Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.

17 BWANA ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye huruma katika matendo yake yote.

18 BWANA yuko karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu.

19 Hutimiza matakwa ya wote wamchao, Na pia husikia kilio chao, na huwaokoa.

20 BWANA huwahifadhi wote wampendao, Na wote wasio haki atawaangamiza.

21 Kinywa changu kitazinena sifa za BWANA; Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu milele na milele.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo