Zaburi 143 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSala ya ukombozi kutoka kwa adui Zaburi ya Daudi. 1 Ee BWANA, uisikie sala yangu, uzisikilize dua zangu Unijibu Kwa uaminifu wako, Unijibu kwa haki yako. 2 Wala usimhukumu mtumishi wako, Maana kwako hakuna aliye hai mwenye haki. 3 Maana adui ameifuatia nafsi yangu, Ameutupa chini uzima wangu. Amenikalisha mahali penye giza, Kama watu waliokufa zamani. 4 Na roho yangu imezimia ndani yangu, Moyo wangu ndani yangu umeshtuka. 5 Nimezikumbuka siku za kale, Nimeyatafakari matendo yako yote, Naziwaza kazi za mikono yako. 6 Nakunyoshea mikono yangu; Nafsi yangu inakuonea kiu kama nchi kame. 7 Ee BWANA, unijibu hima, roho yangu imelegea; Usinifiche uso wako, Nisifanane nao washukao shimoni. 8 Uniwezeshe kusikia fadhili zako asubuhi, Kwa maana nimekutumaini Wewe. Unifundishe njia nitakayoiendea, Kwa maana ninakuinulia nafsi yangu. 9 Ee BWANA, uniponye kutoka kwa adui zangu; Nimekukimbilia Wewe, unifiche. 10 Unifundishe kuyatenda mapenzi yako, Kwa maana ndiwe Mungu wangu; Roho yako mwema aniongoze katika njia iliyo sawa, 11 Ee BWANA, uniponye kwa ajili ya jina lako, Kwa haki yako unitoe roho yangu taabuni; 12 Kwa fadhili zako utawakatilia mbali adui zangu; Na kuwaangamiza wote wanitesao nafsi, Kwa maana mimi ni mtumishi wako. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya