Zaburi 110 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCHakikisho la ushindi kwa mteule wa Mungu Ya Daudi. Zaburi. 1 Neno la BWANA kwa Bwana wangu, Uketi upande wangu wa kulia, Hadi niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako. 2 BWANA atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako. Uwe na enzi kati ya adui zako; 3 Watu wako watajitoa kwa hiari, Siku ya uwezo wako; Kwa uzuri wa utakatifu, Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako. 4 BWANA ameapa, Wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki. 5 Bwana yu mkono wako wa kulia; Atawaponda wafalme, Siku ya ghadhabu yake. 6 Atahukumu kati ya mataifa, Ataijaza nchi mizoga; Atawaponda wakuu katika nchi nyingi. 7 Atakunywa maji ya mto njiani; Kwa hiyo atakiinua kichwa chake kwa ushindi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya