Zaburi 109 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSala ya uthibitisho na kutaka kisasi Kwa mwimbishaji. Ya Daudi. Zaburi. 1 Ee Mungu wa sifa zangu, usinyamaze, 2 Kwa maana vinywa viovu na vyenye hila vimefumbuliwa juu yangu, Vikinisema kwa ulimi wa uongo, Wamesema nami kwa ulimi wa uongo. 3 Naam, kwa maneno ya chuki wamenizunguka, Wamepigana nami bure. 4 Badala ya upendo wangu wao hunishitaki, Ijapokuwa niliwaombea. 5 Wamenilipa mabaya kwa mema yangu, Na chuki badala ya upendo wangu. 6 Umweke mtu mkorofi juu yake, Mshitaki na asimame kulia kwake. 7 Katika kuhukumiwa ataonekana hana haki, Na sala yake itadhaniwa kuwa ni dhambi. 8 Siku zake na ziwe chache, Usimamizi wake na atwae mtu mwingine. 9 Wanawe na wawe yatima, Na mkewe na awe mjane. 10 Kutanga na watange wanawe na kuomba, Watafute chakula mbali na mahame yao. 11 Mdai na anase vitu vyote alivyo navyo, Wageni na wateke mapato ya kazi yake. 12 Asiwe na mtu wa kumfanyia fadhili, Wala mtu wa kuwahurumia yatima wake. 13 Wazawa wake waangamizwe, Jina lao likafutwe katika kizazi cha pili. 14 Uovu wa baba zake ukumbukwe mbele za BWANA, Na dhambi ya mamaye isifutwe. 15 Ziwe mbele za BWANA daima, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. 16 Kwa kuwa hakukumbuka kutenda fadhili, Bali alimfukuza mnyonge na mhitaji, Hata akamwua mtu aliyevunjika moyo, 17 Naye alipenda kulaani, nako kukampata. Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye, 18 Alijivika laana kana kwamba ni vazi lake. Ikamwingilia moyoni kama maji, Na kama mafuta mifupani mwake. 19 Na iwe kwake kama vazi ajivikalo, Na kama mshipi ajifungao daima. 20 Ndiyo malipo ya washitaki wangu toka kwa BWANA, Na ya hao wanaoisingizia nafsi yangu mabaya. 21 Na Wewe, MUNGU, Bwana, unitendee kwa ajili ya jina lako, Kwa kuwa fadhili zako ni njema uniokoe. 22 Kwa maana mimi ni mnyonge na mhitaji, Na moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu. 23 Ninapita kama kivuli kianzacho kutoweka, Ninapeperushwa kama nzige. 24 Magoti yangu yamedhoofu kwa kufunga, Na mwili wangu umekonda kwa kukosa mafuta. 25 Nami nimekuwa wa kudharauliwa na watu, Wanionapo hutikisa vichwa vyao. 26 Ee BWANA, Mungu wangu, unisaidie, Uniokoe kulingana na fadhili zako. 27 Nao wakajue ya kuwa huu ni mkono wako; Wewe, BWANA, umeyafanya hayo. 28 Waache walaani, bali Wewe utabariki, Wanaonishambulia na waaibishwe, Naye mtumishi wako afurahi. 29 Washitaki wangu watavikwa fedheha, Na wavikwe aibu yao kama joho. 30 Nitamshukuru BWANA kwa kinywa changu, Naam, nitamsifu katikati ya mkutano. 31 Maana atasimama mkono wa kulia wa mhitaji Amwokoe kutoka kwa wanaoihukumu nafsi yake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya