Zaburi 102 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSala ya kutaka msaada kutoka kwa Mungu Ombi la anayeteseka, akiwa hoi huku akimlilia BWANA. 1 Ee BWANA, usikie kuomba kwangu, Kilio changu kikufikie. 2 Usinifiche uso wako siku ya shida yangu, Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi. 3 Maana siku zangu zinatoweka kama moshi, Na mifupa yangu inateketea kama kinga. 4 Moyo wangu umepigwa kama majani na kukauka, Naam, ninasahau kula chakula changu. 5 Kwa ajili ya kilio cha kuugua kwangu Mifupa yangu imegandamana na nyama yangu. 6 Nimekuwa kama ndege wa jangwani, Na kufanana na bundi katika mahame. 7 Nakesha, tena nimekuwa kama shomoro Aliye peke yake juu ya nyumba. 8 Adui zangu wananilaumu mchana kutwa; Wanaonichukia kana kwamba wana wazimu Wakitaja jina langu katika laana zao. 9 Maana ninakula majivu kama chakula, Na kukichanganya kinywaji changu na machozi. 10 Kwa sababu ya ghadhabu yako na hasira yako; Maana umeniinua na kunitupilia mbali. 11 Siku zangu ni kama kivuli cha jioni, Nami ninanyauka kama majani. 12 Bali Wewe, BWANA utaketi ukimiliki milele, Na jina lako litakumbukwa na vizazi vyote. 13 Wewe mwenyewe utasimama, Na kuirehemu Sayuni, Kwa maana ndio wakati wa kuihurumia, Naam, majira yaliyoamriwa yamewadia. 14 Maana watumishi wako wameyaridhia mawe yake, Na kuyaonea huruma mavumbi yake. 15 Kisha mataifa wataliogopa jina la BWANA, Na wafalme wote wa dunia utukufu wako; 16 BWANA atakapokuwa ameijenga Sayuni, Atakapoonekana katika utukufu wake, 17 Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa, Asiyadharau maombi yao. 18 Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo, Na watu watakaoumbwa watamsifu BWANA. 19 Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu, Toka mbinguni BWANA ameiangalia nchi, 20 Ili akisikie kilio cha kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa. 21 Watu walitangaze jina la BWANA katika Sayuni, Na sifa zake katika Yerusalemu, 22 Pindi mataifa watapokusanyika pamoja, Na falme, ili kumtumikia BWANA. 23 Amezipunguza nguvu zangu njiani; Amezifupisha siku zangu. 24 Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu; Miaka yako ni tangu kizazi hata kizazi. 25 Hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi, Na mbingu ni kazi ya mikono yako. 26 Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu Naam, hizi zitachakaa kama nguo; Na kama mavazi utazibadilisha, Nazo zitabadilika. 27 Lakini Wewe U Yeye yule; Na miaka yako haina mwisho. 28 Wana wa watumishi wako watakaa, Na wazawa wao wataimarishwa mbele zako. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya