Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Yobu 42 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Ayubu anyenyekezwa na kutoshelezwa

1 Ndipo Ayubu akamjibu BWANA, na kusema.

2 Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.

3 Ni nani huyu afichaye ushauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, Mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua.

4 Sikiliza, nakusihi, nami nitanena; Nitakuuliza neno, nawe niambie.

5 Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona.

6 Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu Katika mavumbi na majivu.


Marafiki wa Ayubu waaibishwa

7 Basi ikawa, baada ya BWANA kumwambia Ayubu maneno hayo, BWANA akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.

8 Basi sasa, jitwalieni ng'ombe dume saba, na kondoo dume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende kulingana na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.

9 Basi Elifazi, Mtemani, na Bildadi, Mshuhi, na Sofari, Mnaamathi, wakaenda, wakafanya kama vile BWANA alivyowaamuru; naye BWANA akamridhia Ayubu.


Ayubu arejeshewa mali yake maradufu

10 Kisha BWANA akamrejeshea Ayubu mali yake, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza.

11 Ndipo wakamwendea ndugu zake wote, wanaume kwa wanawake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakampa pole na kumliwaza kwa ajili ya mateso hayo yote aliyoleta BWANA juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja.

12 Basi hivyo BWANA akaubariki huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu moja, na punda wake elfu moja.

13 Tena alikuwa na watoto wa kiume saba, na binti watatu.

14 Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu.

15 Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao wa kiume.

16 Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia moja na arubaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hadi kizazi cha nne.

17 Basi Ayubu akafa, akiwa mzee sana mwenye kujawa na siku.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo