Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Yobu 40 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC

1 BWANA akafululiza kumjibu Ayubu, na kusema,

2 Je! Mwenye hoja atashindana na Mwenyezi? Mwenye kujadiliana na Mungu, na ajibu yeye.


Jibu la Ayubu kwa Mungu

3 Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema,

4 Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu.

5 Nimenena mara moja, nami sitajibu; Naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.


Mungu amchochea Ayubu

6 Ndipo BWANA akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema,

7 Jifunge viuno kama mwanamume, Mimi nitakuuliza neno, nawe niambie.

8 Je! Hata hukumu yangu utaibatilisha? Utanitia mimi hatiani, upate kuhesabiwa haki?

9 Au je! Wewe una mkono kama Mungu? Waweza kutoa ngurumo kwa sauti kama yeye?

10 Haya! Jivike sasa fahari na ukuu; Jipambe heshima na enzi.

11 Mwaga mafuriko ya hasira zako, Ukamtazame kila mtu mwenye kiburi, ukamdhalilishe.

12 Mtazame kila mtu mwenye kiburi ukamshushe, Ukawakanyage waovu hapo wasimamapo.

13 Wafiche mavumbini pamoja, Wafunge nyuso zao mahali palipositirika.

14 Ndipo mimi nami nitazikiri habari zako, Ya kuwa mkono wako wa kulia waweza kukuokoa.

15 Mwangalie huyo kiboko, niliyemwumba pamoja nawe; Yeye hula nyasi kama ng'ombe,

16 Tazama basi, nguvu zake zimo katika viuno vyake, Na uwezo wake u katika mishipa ya tumbo lake.

17 Yeye hutikisa mkia wake mfano wa mwerezi; Mishipa ya mapaja yake yanaungamana pamoja.

18 Mifupa yake ni kama mirija ya shaba; Mbavu zake ni kama vipande vya chuma.

19 Yeye ni wa kwanza kwa hayo matendo makuu ya Mungu; Ni Muumba wake tu awezaye kumkabili kwa upanga wake.

20 Hakika milima humtolea chakula; Hapo wachezapo wanyama pori wote.

21 Hulala chini ya miti yenye vivuli, Mafichoni penye mianzi, na matopeni.

22 Hiyo miti yenye vivuli humfunika kwa vivuli vyao; Mierebi ya vijito humzunguka.

23 Tazama, mto ukifurika, yeye hatetemeki; Hujiona yu salama, ijapokuwa Yordani hufurika hata kinywani pake.

24 Je! Mtu yeyote atamnasa akiwa yu macho, Au, kumtoboa pua yake kwa mtego?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo