Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Yobu 4 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Elifazi anena: Ayubu ametenda dhambi

1 Ndipo huyo Elifazi, Mtemani, akajibu na kusema,

2 Mtu akijaribu kuzungumza nawe, je! Utaona ni vibaya? Lakini ni nani awezaye kujizuia asinene?

3 Tazama, wewe umewafunza watu wengi, Nawe umeitia nguvu mikono iliyokuwa minyonge.

4 Maneno yako yamemtegemeza huyo aliyekuwa anaanguka, Nawe umeyaimarisha magoti manyonge.

5 Lakini sasa haya yamekufikia wewe, nawe wafa moyo; Yamekugusa, nawe wafadhaika.

6 Je! Dini yako siyo tegemeo lako? Na matumaini yako si huo uelekevu wa njia zako?

7 Kumbuka, tafadhali, ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia? Au ni wapi hao waelekevu walikatiliwa mbali?

8 Kama mimi nilivyoona, hao walimao maovu, Na kupanda madhara, huvuna yayo hayo.

9 Kwa pumzi za Mungu huangamia. Na kwa kuvuma kwa hasira zake humalizika.

10 Kunguruma kwake simba, na sauti ya simba mkali, Na meno ya simba wachanga, yamevunjika.

11 Simba mzee huangamia kwa kukosa mawindo, Nao watoto wa simba jike wametawanyika mbalimbali.

12 Basi, nililetewa neno kwa siri, Sikio langu likasikia manong'ono yake.

13 Katika mawazo yaliyotoka katika maono ya usiku, Hapo usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu.

14 Hofu iliniangukia na kutetemeka, Iliyoitetemesha mifupa yangu yote.

15 Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; Na nywele za mwili wangu zilisimama.

16 Hiyo pepo ilisimama kimya, nisiweze kutambua sura zake, Mfano ulikuwa mbele ya macho yangu; Kulikuwa kimya, nami nilisikia sauti, ikinena,

17 Je! Binadamu atakuwa na haki kuliko Mungu? Je! Mtu atakuwa safi kuliko Muumba wake?

18 Tazama, yeye hawategemei watumishi wake; Na malaika wake huwahesabia kosa;

19 Je! Si zaidi sana hao wakaao katika nyumba za udongo, Ambazo misingi yao i katika mchanga, Hao wanaopondwa kama nondo!

20 Kati ya asubuhi na jioni huvunjwa-vunjwa; Waangamia milele wala hapana atiaye moyoni.

21 Je! Kamba ya hema yao haikung'olewa ndani yao? Nao hufa hata bila kuwa na hekima.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo