Yobu 36 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCElihu asifia wema wa Mungu 1 Tena Elihu akaendelea na kusema, 2 Ningojee kidogo nami nitakueleza; Kwa kuwa ningali na maneno kwa ajili ya Mungu. 3 Nitayaleta maarifa yangu kutoka mbali, Nami nitampa haki Muumba wangu. 4 Maana hakika maneno yangu si ya uongo; Aliyekamilika katika maarifa yu pamoja nawe. 5 Tazama, Mungu ni hodari, wala hamdharau mtu yeyote; Ana uweza katika nguvu za fahamu. 6 Hauhifadhi uhai wa waovu; Lakini huwapa wateswao haki yao. 7 Yeye hawaondolei macho yake wenye haki; Lakini pamoja na wafalme huwaweka Katika viti vya enzi milele, nao hutukuzwa. 8 Nao wakifungwa kwa pingu, Wakitwaliwa kwa kamba za mateso; 9 Ndipo huwaonesha matendo yao, Na makosa yao, ya kuwa wametenda kwa kujivuna. 10 Yeye huyafunua masikio yao, wasikie maonyo, Na kuwaagiza warudi kuuacha uovu. 11 Kama wakisikia na kumtumikia, Watapisha siku zao katika kufanikiwa, Na miaka yao katika furaha. 12 Lakini wasiposikia, wataangamia kwa upanga, Nao watakufa pasipo maarifa. 13 Lakini hao wasiomcha Mungu mioyoni hujiwekea hasira Hawalilii msaada hapo awafungapo. 14 Wao hufa wakingali vijana, Na uhai wao huangamia katikati ya wachafu. 15 Yeye humponya aliyetaabika kwa njia ya taabu yake, Na kuyafunua masikio yao kwa maonevu. 16 Naam, yeye angekuongoza utoke katika msiba Hata mahali penye nafasi, ambapo hapana kizuizi; Na kilichowekwa mezani pako kingejaa mafuta. 17 Lakini umejaa hukumu ya waovu; Hukumu na haki hukushika. 18 Basi ujitunze, isije hasira ikakuvuta hata ukafanya mzaha; Wala usikubali ukuu wa ukombozi ukugeuze. 19 Je! Mali yako itatosha, hata usiwe katika taabu, Au uwezo wote wa nguvu zako? 20 Usiutamani usiku, Wakati watu wakatwapo katika mahali pao. 21 Jitunze, usiutazame uovu; Kwani umeuchagua huo zaidi ya taabu. 22 Tazama, Mungu hutenda makuu kwa uweza wake; Ni nani afundishaye kama yeye? 23 Ni nani aliyemwagiza njia yake? Au ni nani awezaye kusema, Wewe umetenda yasiyo haki? Elihu atangaza ukuu wa Mungu 24 Kumbuka kuitukuza kazi yake, Watu waliyoiimbia. 25 Wanadamu wote wameitazama; Watu huiangalia kwa mbali. 26 Tazama, Mungu ni mkuu, nasi hatumjui; Hesabu ya miaka yake haichunguziki. 27 Maana yeye huvuta juu matone ya maji, Yamwagikayo katika mvua kutoka ukungu wake; 28 Ambayo mawingu yainyesha Na kudondoza juu ya wanadamu kwa wingi. 29 Naam, mtu aweza kuelewa matandazo ya mawingu, Ngurumo za makao yake? 30 Tazama, yeye huutandaza mwanga wake, umzunguke; Naye hufunika vilindi vya bahari. 31 Kwani huwahukumu makabila ya watu kwa njia hizi; Hutoa chakula kwa ukarimu. 32 Yeye huifunika mikono yake kwa umeme; Na kuuagiza shabaha utakayopiga. 33 Mshindo wake hutoa habari zake, Anayewaka hasira juu ya uovu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya