Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Yobu 29 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Ayubu amalizia hoja zake

1 Kisha Ayubu akaendelea na hoja yake, na kusema,

2 Laiti ningekuwa kama nilivyokuwa katika miezi ya zamani, Kama katika siku hizo Mungu aliponilinda;

3 Hapo taa yake ilipomulika juu yangu kichwani, Nami nilitembea gizani kwa njia ya mwanga wake;

4 Kama nilivyokuwa katika siku zangu za kukomaa, Hapo siri ya Mungu ilipokuwa hemani mwangu;

5 Wakati Mwenyezi alipokuwa angali pamoja nami, Nao watoto wangu walipokuwa wakinizunguka;

6 Wakati hatua zangu zilipokuwa zikioshwa kwa siagi, Nalo jabali liliponimiminia mito ya mafuta!

7 Wakati nilipotoka kwenda mjini, kupitia langoni, Nilipokitengeza kiti changu katika njia kuu,

8 Hao vijana waliniona wakanipisha, Nao wazee wakasimama kwa heshima;

9 Wakuu wakanyamaa wasinene, Na kuweka mikono yao vinywani mwao;

10 Sauti yao wakuu ilinyamaa, Na ndimi zao zilishikamana na makaakaa yao.

11 Maana sikio liliponisikia, ndipo likanibarikia; Na jicho liliponiona, likanishuhudia.

12 Kwa sababu nilimwokoa maskini aliyenililia; Yatima naye, na yule asiyekuwa na mtu wa kumsaidia.

13 Baraka yake yeye aliyekuwa karibu na kupotea ilinijia; Nikaufanya moyo wa mjane kuimba kwa furaha.

14 Nilijivika haki, ikanifunika, Adili yangu ilikuwa kama joho na kilemba.

15 Nilikuwa macho kwa kipofu, Nilikuwa miguu kwa aliyechechemea.

16 Nilikuwa baba kwa mhitaji, Na kesi ya mtu nisiyemjua niliichunguza.

17 Nami nilizivunja taya za wasio haki, Na kumpokonya mawindo katika meno yake.

18 Ndipo niliposema, Nitakufa ndani ya kiota changu, Nami nitaziongeza siku zangu kama mchanga;

19 Shina langu limeenea hata kufika majini, Na umande hukaa usiku kucha katika matawi yangu;

20 Utukufu wangu utakuwa mpya kwangu, Na uta wangu hurejeshwa upya mkononi mwangu.

21 Watu walitega masikio kunisikiliza, na kungoja, Wakanyamaza kimya wapate kusikia mashauri yangu.

22 Hawakunena tena baada ya kusikia maneno yangu; Matamko yangu yakadondoka juu yao.

23 Walikuwa wakiningojea kama kungojea mvua; Wakafunua vinywa vyao sana kama mvua ya masika.

24 Walipokata tamaa nikacheka nao; Na mwanga wa uso wangu hawakuuangusha.

25 Niliwachagulia njia, nikakaa kama mkuu wao. Nikakaa kama mfalme katika jeshi la askari, Mfano wa awafarijiye hao waombolezao.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo