Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Yobu 20 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Sofari anena: Uovu hupatilizwa ipasavyo

1 Ndipo Sofari, Mnaamathi, akajibu, na kusema,

2 Kwa hiyo mawazo yangu hunipa jawabu, Kwa ajili ya haraka niliyo nayo ndani yangu.

3 Nimesikia maonyo yanayonitahayarisha, Nayo roho ya ufahamu wangu hunijibu.

4 Je! Hujui neno hili tangu zamani za kale, Tangu wanadamu kuwekwa juu ya nchi,

5 Ya kuwa shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo, Na furaha ya wapotovu ni ya dakika moja tu?

6 Ujapopanda ukuu wake mpaka mbinguni, Na kichwa chake kufikia mawinguni;

7 Hata hivyo ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe; Hao waliomwona watasema, Yuko wapi?

8 Ataruka mfano wa ndoto, asionekane; Naam, atafukuzwa kama maono ya usiku,

9 Jicho lililomwona halitamwona tena; Wala mahali pake hapatamtazama tena.

10 Watoto wake watataka fadhili kwa maskini, Na mikono yake itarudisha mali yake.

11 Mifupa yake imejaa ujana wake, Lakini utalala nchi naye mavumbini.

12 Ingawa uovu ni mtamu kinywani mwake, Ingawa auficha chini ya ulimi wake;

13 Ingawa hawataki kuuachilia uende zake. Naye huushikilia kinywani mwake;

14 Hata hivyo chakula chake matumboni mwake kinabadilika, Kimekuwa ni nyongo za majoka ndani yake.

15 Amemeza mali, naye atayatapika tena; Mungu atayatoa tumboni mwake.

16 Atanyonya sumu ya majoka; Na ulimi wa fira utamwua.

17 Hataiangalia hiyo mito ya maji, Vile vijito vilivyojaa asali na siagi.

18 Aliyoyataabikia kazi atayarudisha, asiyameze; Kwa mali aliyoyapata, hatafurahi.

19 Kwa maana amewaonea na kuwaacha maskini; Amenyang'anya nyumba kwa jeuri, wala hataijenga.

20 Kwa sababu hakujua utulivu ndani yake, Hataokoa chochote kutoka hicho alichokifurahia.

21 Hakikusalia kitu asichokula; Kwa hiyo kufanikiwa kwake hakutadumu.

22 Katika kujaa kwa wingi wake atakuwa katika dhiki; Mkono wa kila anayesumbuliwa utamjia.

23 Hapo atakapo kulijaza tumbo lake, Mungu atamtupia ukali wa ghadhabu zake, Na kuunyesha juu yake akiwa anakula.

24 Ataikimbia silaha ya chuma, Na uta wa shaba utamchoma.

25 Yeye autoa, nao watoka mwilini mwake; Naam, ncha ing'aayo yatoka katika nyongo yake; Vitisho viko juu yake.

26 Giza lote linawekwa kwa ajili ya hazina zake; Moto ambao haukuvuviwa na mtu utamla; Utayateketeza yaliyosalia hemani mwake.

27 Mbingu zitafunua wazi uovu wake, Nayo nchi itainuka kinyume chake.

28 Mali ya nyumba yake yatanyakuliwa, Yatamwagika mbali katika siku ya ghadhabu zake.

29 Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu itokayo kwa Mungu, Na urithi aliowekewa na Mungu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo