Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Yobu 2 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Pigo kwa afya ya Ayubu

1 Tena ilitukia siku moja hao wana wa Mungu walipokwenda kujiweka mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujiweka mbele za BWANA.

2 BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi? Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzungukazunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.

3 BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hakuna hata mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ijapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu.

4 Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake.

5 Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako.

6 BWANA akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake.

7 Basi Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hadi utosi wa kichwa.

8 Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni.

9 Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Mkufuru Mungu, ufe.

10 Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.


Marafiki watatu wa Ayubu

11 Basi ikawa hao marafiki watatu wa Ayubu walipopata habari ya mabaya hayo yote yaliyomfikia, wakaja kila mtu kutoka mahali pake; nao ni Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi; wakapatana pamoja ili waende kumfariji Ayubu na kumtuliza moyo.

12 Basi walipoinua macho yao, wakiwa bado kwa mbali, wasimtambue, wakainua sauti zao na kulia; kila mmoja akararua joho lake, wakarusha mavumbi juu ya vichwa vyao kuelekea mbinguni.

13 Kisha wakaketi ardhini pamoja naye muda wa siku saba, mchana na usiku, wala hapana mmoja aliyenena naye neno lolote; kwa maana waliona ya kuwa mashaka yake aliyo nayo ni makuu mno.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo