Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Yeremia 49 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Hukumu juu ya Waamoni

1 Kuhusu wana wa Amoni. BWANA asema hivi, Je, Israeli hana wana? Je! Hana mrithi? Basi, mbona Malkamu anamiliki Gadi, na watu wake wanakaa katika miji yake?

2 Basi, kwa sababu hiyo, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya kishindo cha vita kisikike juu ya Raba, mji wa Amoni, nao utakuwa magofu ya ukiwa, na binti zake watateketezwa kwa moto; ndipo Israeli watawamiliki wao waliokuwa wakimmiliki, asema BWANA.

3 Omboleza, Ee Heshboni, Kwa maana Ai umeangamizwa; Lieni, enyi binti za Raba, Mjivike nguo za magunia; Ombolezeni, mkipiga mbio Huko na huko kati ya maboma; Maana Malkamu atakwenda kuhamishwa, Makuhani wake na wakuu wake pamoja.

4 Mbona unajisifu kwa sababu ya mabonde, bonde lako litiririkalo, Ee binti mwenye kuasi? Utumainiaye hazina zako, ukisema, Ni nani atakayenijia?

5 Tazama, nitaleta hofu juu yako, asema Bwana, BWANA wa majeshi, itakayotoka kwa wote wakuzungukao; nanyi mtafukuzwa nje, kila mtu mbali kabisa, wala hapana mtu wa kuwakusanya wapoteao.

6 Lakini baada ya hayo nitawarudisha wana wa Amoni walio utumwani, asema BWANA.


Hukumu juu ya Edomu

7 Kuhusu Edomu. BWANA wa majeshi asema hivi, Je! Hakuna tena hekima katika Temani? Mashauri yamewapotea wenye busara? Je! Imetoweka hekima yao?

8 Kimbieni, rudini nyuma, kaeni chini sana, enyi mnaokaa Dedani; maana nitaleta msiba wa Esau juu yake, wakati nitakapomwangalia.

9 Je! Kama wachuma zabibu wangekujia, wasingeacha zabibu ziokotwe? Kama wangekujia wezi usiku, wasingeharibu hata watakapopata vya kutosha?

10 Lakini nimemwacha akiwa hana kitu Esau, nimepafunua mahali pake pa siri, wala hataweza kujificha; kizazi chake kimeangamizwa, na ndugu zake, na jirani zake, naye mwenyewe hayuko.

11 Waache watoto wako wasio na baba, mimi nitawahifadhi hai, na wajane wako na wanitumaini mimi.

12 Maana BWANA asema hivi, Tazama, wale wasioandaliwa kunywea kikombe, watakinywea, ni hakika; na wewe je! U mtu ambaye hataadhibiwa kabisa? Hukosi utaadhibiwa, naam, kunywa utakunywa.

13 Kwa maana nimeapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, kwamba Bozra utakuwa ajabu, na aibu, na ukiwa, na laana; na miji yake yote itakuwa ukiwa wa daima.

14 Nimepata habari kwa BWANA, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema, Jikusanyeni, mkaujie, Mkainuke kwenda vitani.

15 Maana nimekufanya mdogo kati ya mataifa, Na kudharauliwa katika watu.

16 Kuhusu kuogofya kwako, Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Ushikaye kilele cha milima; Ujapofanya kiota chako juu sana kama tai, Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA.

17 Na Edomu atakuwa ajabu; kila mtu apitaye atashangaa, na kuzomea, kwa sababu ya mapigo yake yote.

18 Kama vile vilivyotokea wakati wa kuangushwa Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema BWANA; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo.

19 Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafla ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu?

20 Basi, lisikieni shauri la BWANA; Alilolifanya juu ya Edomu; Na makusudi yake aliyoyakusudia Juu yao wakaao Temani; Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi; Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao.

21 Nchi yatetemeka kwa sauti ya kuanguka kwao; Kuna kilio, sauti yake yasikiwa katika Bahari ya Shamu.

22 Tazama, atapanda na kuruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Bozra; na mioyo ya mashujaa wa Edomu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke akiwa katika uchungu wa kujifungua.


Hukumu juu ya Dameski

23 Kuhusu Dameski. Hamathi umetahayarika, na Arpadi pia; Maana wamesikia habari mbaya; Wameyeyuka kabisa; Wamesumbuka kama bahari, isiyoweza kutulia.

24 Dameski umedhoofika; Umejigeuza kukimbia; tetemeko limeushika; Dhiki na huzuni zimeupata, Kama za mwanamke katika uchungu wake.

25 Imekuwaje mji wa sifa haukuachwa, mji wa furaha yangu?

26 Kwa hiyo vijana wake wataanguka katika njia zake kuu, na watu wote wa vita watanyamazishwa katika siku hiyo, asema BWANA wa majeshi.

27 Nami nitawasha moto katika ukuta wa Dameski, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi.


Hukumu juu ya Kedari na Hazori

28 Kuhusu Kedari, na falme za Hazori, ambazo Nebukadneza, mfalme wa Babeli, alizipiga. BWANA asema hivi, Ondokeni, pandeni hadi Kedari, mkawateke nyara wana wa mashariki.

29 Hema zao na makundi yao watayatwaa; watachukulia mbali mapazia yao kwa faida yao wenyewe, na vyombo vyao vyote, na ngamia wao; nao watawapigia kelele wakisema, Hofu ziko pande zote.

30 Kimbieni ninyi, nendeni mbali mkitangatanga, kaeni chini sana, enyi mkaao Hazori, asema BWANA; maana Nebukadneza, mfalme wa Babeli, amefanya shauri juu yenu, naye amekusudia neno juu yenu.

31 Ondokeni, pandeni hata taifa lililo katika hali ya raha, likaalo bila kuhangaika, asema BWANA; wasio na malango wala makomeo, wakaao peke yao.

32 Na ngamia wao watakuwa mateka, na wingi wa makundi yao utakuwa nyara; nami nitawatawanya katika pande zote watu wale wanyoao denge; nami nitaleta msiba wao toka pande zao zote, asema BWANA.

33 Na Hazori utakuwa kao la mbwamwitu; ukiwa milele; hakuna mtu atakayekaa huko, wala hakuna mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo.


Hukumu juu ya Elamu

34 Neno la BWANA lililomjia Yeremia, nabii, juu ya Elamu, mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, kusema,

35 BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama nitauvunja upinde wa Elamu, ulio mkuu katika nguvu zao.

36 Na juu ya Elamu nitazileta pepo nne, toka pembe nne za mbinguni, nami nitawatawanya katika pande zote nne, wala hakuna taifa ambalo hawatalifikia watu wa Elamu waliofukuzwa.

37 Nami nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya adui zao, na mbele ya hao wanaowatafuta roho zao; nami nitawaletea mabaya, naam, hasira yangu kali, asema BWANA; nami nitautuma upanga uwafuatie, hadi nitakapowaangamiza;

38 nami nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu, nami nitawaharibu, mfalme na wakuu, watoke huko, asema BWANA.

39 Lakini itakuwa, katika siku za mwisho, nitawarudisha wafungwa wa Elamu, asema BWANA.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo