Yeremia 2 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCMungu awasihi Waisraeli watubu 1 Neno la BWANA likanijia, kusema, 2 Nenda ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, BWANA asema hivi, Nakukumbuka, hisani ya ujana wako, upendo wa wakati wa kuposwa kwako; Jinsi ulivyonifuata huko jangwani, katika nchi isiyopandwa mbegu. 3 Israeli walikuwa utakatifu kwa BWANA; malimbuko ya uzao wake; Wote watakaomla watakuwa na hatia; uovu utawajia; asema BWANA. 4 Lisikieni neno la BWANA, ninyi nyumba ya Yakobo, na ninyi, jamaa zote za nyumba ya Israeli. 5 BWANA asema hivi, Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu, hata wakafarakana nami, wakafuata ubatili, nao wakawa ubatili? 6 Wala hawakusema, Yuko wapi BWANA, aliyetutoa katika nchi ya Misri; akatuongoza jangwani, katika nchi ya ukame na mashimo, katika nchi ya kiu na ya kivuli cha mauti, katika nchi ambayo ndani yake hapiti mtu, wala haikukaliwa na watu? 7 Nami nikawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu mliufanya kuwa chukizo. 8 Makuhani hawakusema, Yuko wapi BWANA? Wala wanasheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu. 9 Basi, kwa ajili ya hayo nitateta nanyi, asema BWANA, nami nitateta na watoto wa watoto wenu. 10 Maana, vukeni mpaka visiwa vya Kitimu, mkaone; tumeni watu waende Kedari, mkafikiri sana; mkaone kwamba jambo kama hili limekuwa wakati wowote. 11 Je! Taifa wamebadili miungu yao, ingawa siyo miungu? Lakini watu wangu wameubadili utukufu wao kwa ajili ya kitu kisichofaidia. 12 Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope sana, na kuwa ukiwa sana, asema BWANA. 13 Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia visima, visima vyenye nyufa visivyoweza kuweka maji. 14 Je! Israeli ni mtumwa? Je! Ni mzalia? Mbona amekuwa mateka? 15 Wanasimba wamenguruma juu yake, wametoa sana sauti zao; Nao wameifanya nchi yake kuwa ukiwa; miji yake imeteketea, haina watu. 16 Tena wana wa Nofu na Tapanesi wamevunja utosi wa kichwa chako. 17 Je! Hukujipatia mambo haya mwenyewe, kwa kuwa umemwacha BWANA, Mungu wako, alipokuongoza njiani? 18 Na sasa una nini utakayofaidi katika njia iendayo Misri, kunywa maji ya Shihori? Au una nini utakayofaidi katika njia iendayo Ashuru, kunywa maji ya ule Mto? 19 Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha BWANA, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, BWANA wa majeshi. 20 Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba. 21 Nami nilikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibumwitu machoni pangu? 22 Maana ujapojiosha kwa magadi, na kujipatia sabuni nyingi, lakini uovu wako umeandikwa mbele zangu, asema Bwana MUNGU. 23 Wawezaje kusema, Sikutiwa unajisi, sikuwafuata Mabaali? Itazame njia yako bondeni, ujue uliyoyatenda; wewe u ngamia mwepesi, apitaye katika njia zake; 24 punda wa mwitu aliyeizoelea nyika, avutaye pumzi za upepo katika tamaa yake; katika wakati wake ni nani awezaye kumgeuza? Wote wamtafutao hawatajichosha nafsi zao; katika mwezi wake watamwona. 25 Zuia mguu wako usikose kiatu, na koo yako isiwe na kiu; lakini wewe ulisema, Hakuna matumaini kabisa; la, maana nimewapenda wageni, nami nitawafuata. 26 Kama mwizi aonavyo haya akamatwapo, ndivyo waonavyo haya nyumba ya Israeli; wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao; 27 waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe. 28 Lakini wako wapi miungu yako ulioifanya? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda. 29 Mbona mnataka kuteta nami? Ninyi nyote mmeniasi, asema BWANA. 30 Nimewapiga watoto wako bure; hawakukubali kurudiwa; upanga wenu wenyewe umewala manabii wako, kama simba aharibuye. 31 Ee kizazi litazameni neno la BWANA. Je! Nimekuwa jangwa kwa Israeli? Au nchi yenye giza kuu? Mbona watu wangu wanasema, Sisi tumetoroka, hatutaki kuja kwako tena? 32 Je! Mwanamwali aweza kusahau mapambo yake, au bibi arusi mavazi yake? Lakini watu wangu wamenisahau mimi kwa muda wa siku zisizo na hesabu. 33 Jinsi ulivyoitengeneza njia yako ili kutafuta mapenzi! Kwa sababu hiyo hata wanawake wabaya umewafundisha njia zako. 34 Tena katika pindo za nguo zako imeonekana damu ya roho zao maskini wasio na hatia; sikuiona penye mahali palipobomoka, lakini niliiona juu ya hawa wote. 35 Lakini ulisema, Sina hatia mimi; bila shaka hasira yake imegeuka na kuniacha. Tazama, nitaingia hukumuni pamoja nawe, kwa sababu unasema, Sikutenda dhambi mimi. 36 Mbona unatangatanga hivi upate kugeuza mwendo wako? Utaona haya kwa ajili ya Misri pia, kama ulivyoona haya kwa ajili ya Ashuru. 37 Hata kwake pia utatoka, na mikono yako juu ya kichwa chako; kwa maana BWANA amewakataa uliowakimbilia, wala hutafanikiwa katika hao. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya