Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Wimbo Ulio Bora 4 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Uzuri wa bibi arusi watukuzwa

1 Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua, Nyuma ya barakoa yako. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi, Wakijilaza mbavuni pa mlima Gileadi.

2 Meno yako ni kama kundi waliokatwa manyoya, Wakipanda kutoka kuoshwa, Ambao kila mmoja amezaa mapacha, Wala hakuna aliyefiwa kati yao.

3 Midomo yako ni kama uzi mwekundu, Na kinywa chako ni kizuri; Mashavu yako ni kama nusu kipande cha komamanga, Nyuma ya barakoa yako.

4 Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, Uliojengwa pa kuwekea silaha; Ngao elfu zimetungikwa juu yake, Zote ni ngao za mashujaa.

5 Matiti yako mawili ni kama wanapaa wawili, Nyuma ya barakoa yako. Ambao ni mapacha ya paa; Wakilisha penye nyinyoro.

6 Hata jua lipunge, na vivuli vikimbie, Nitakwenda kwenye mlima wa manemane, Na kwenye kilima cha ubani.

7 Mpenzi wangu, u mzuri kwa ujumla, Wala ndani yako hamna kasoro.

8 Bibi arusi, njoo pamoja nami toka Lebanoni, Pamoja nami toka Lebanoni. Shuka kutoka kilele cha Amana, Kutoka vilele vya Seniri na Hermoni; Kutoka mapangoni mwa simba, Kutoka milimani mwa chui.

9 Umenishangaza moyo, dada yangu, Bibi arusi, umenishangaza moyo, Kwa mtupo mmoja wa macho yako, Kwa mkufu mmoja wa shingo yako.

10 Jinsi pendo lako lilivyo nzuri, dada yangu, Bibi arusi, ni nzuri kupita divai; Na harufu ya marhamu yako Yapita manukato ya kila namna.

11 Bibi arusi, midomo yako yadondosha asali, Asali na maziwa viko chini ya ulimi wako; Na harufu ya mavazi yako Ni kama harufu ya Lebanoni.

12 Bustani iliyofungwa ni dada yangu, bibi arusi, Kijito kilichofungwa, chemchemi iliyotiwa mhuri.

13 Machipuko yako ni bustani ya komamanga, Yenye matunda mazuri, hina na nardo,

14 Nardo na zafarani, mchai na mdalasini, Na miti yote iletayo ubani, Manemane na udi, na kolezi kuu zote.

15 Wewe ndiwe chemchemi ya bustani yangu, Kisima cha maji yaliyo hai, Vijito vya Lebanoni viendavyo kasi.

16 Amka, kaskazi; nawe uje, kusi; Vumeni juu ya bustani yangu, Manukato ya bustani yatokee. Mpendwa wangu na aingie bustanini mwake, Akayale matunda yake mazuri.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo