Wimbo Ulio Bora 3 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCNdoto za mapenzi 1 Usiku kitandani nilimtafuta mpendwa wa nafsi yangu, Nilimtafuta, nisimpate. 2 Nikasema, Haya, niondoke nizunguke mjini, Katika njia zake na viwanjani, Nimtafute mpendwa wa nafsi yangu. Nikamtafuta, nisimpate. 3 Walinzi wazungukao mjini waliniona; Je! Mmemwona mpendwa wa nafsi yangu? 4 Kitambo kidogo tu nilipoachana nao, Nikamwona mpendwa wa nafsi yangu; Nikamshika, nisimwache tena, Hata nilipomleta nyumbani mwa mamangu, Chumbani mwake aliyenizaa. 5 Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe. Bwana arusi na kundi lake wakaribia 6 Ni nani huyu apandaye kutoka nyikani, Mfano wake ni nguzo za moshi; Afukizwa manemane na ubani, Na mavumbi ya manukato yote ya mchuuzi? 7 Tazama, ni machela yake Sulemani; Mashujaa sitini waizunguka, Wa mashujaa wa Israeli. 8 Wote wameshika upanga, Wamehitimu kupigana; Kila mtu anao upanga wake pajani Kwa hofu ya kamsa za usiku. 9 Mfalme Sulemani alijitengenezea machela Ya miti ya Lebanoni; 10 Nguzo zake alizitengeneza za fedha, Na mgongo wake wa dhahabu, Kiti chake kimepambwa urujuani, Gari lake limenakishiwa njumu, Hiba ya binti za Yerusalemu. 11 Tokeni, enyi binti za Sayuni, Mtazameni Mfalme Sulemani, Amevaa taji alilovikwa na mamaye, Siku ya posa yake, Siku ya furaha ya moyo wake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya