Wimbo Ulio Bora 2 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC1 Mimi ni ua la uwandani, Ni fahirisi ya mabondeni. 2 Kama fahirisi kati ya miiba, Kadhalika mpenzi wangu kati ya binti. 3 Kama mpera kati ya miti ya msituni, Kadhalika mpendwa wangu kati ya vijana. Niliketi kivulini mwake kwa furaha, Na matunda yake niliyaonja kuwa matamu. 4 Akanileta mpaka nyumba ya karamu, Na bendera yake juu yangu ni mapenzi. 5 Nishibisheni zabibu, niburudisheni kwa mapera, Kwa maana nimezimia kwa mapenzi. 6 Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, Nao wa kulia unanikumbatia! 7 Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe. 8 Sikiliza! Ni mpendwa wangu! Tazama, anakuja, Akiruka milimani, akichachawa vilimani. 9 Mpendwa wangu ni kama paa, au ayala. Tazama, asimama nyuma ya ukuta wetu, Achungulia dirishani, atazama kimiani. 10 Mpendwa wangu alinena, akaniambia, Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako, 11 Maana tazama, majira ya baridi yamepita, Masika imekwisha, imekwenda zake; 12 Maua yatokea katika nchi, Wakati wa kuimba umefika, Na sauti ya mwigo husikiwa kwetu. 13 Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa harufu yake nzuri; Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako. 14 Hua wangu, mafichoni mwa jabali, Katika sitara za, magenge Nitazame uso wako, nisikie sauti yako, Maana sauti yako ni tamu na uso wako unapendeza. 15 Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua. 16 Mpendwa wangu ni wangu, na mimi ni wake; Hulisha kundi lake penye nyinyoro. 17 Hata jua lipunge, na vivuli vikimbie, Unigeukie, mpendwa wangu, Nawe uwe kama paa, au ayala, Juu ya milima ya Betheri. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya