Walawi 24 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCTaa isiyozimika 1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 2 Waagize wana wa Israeli wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima. 3 Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeneza tangu jioni hadi asubuhi mbele za BWANA daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu. 4 Atazitengeneza hizo taa katika kile kinara kilicho safi mbele za BWANA daima. Mikate ya Hema Takatifu 5 Nawe utatwaa unga mwembamba, na kuoka mikate kumi na miwili ya huo unga; sehemu za kumi mbili za efa, zitakuwa katika mkate mmoja. 6 Nawe iweke mistari miwili, mikate sita kwa kila mstari, juu ya hiyo meza safi, mbele za BWANA. 7 Nawe utatia ubani safi juu ya kila mstari, ili uwe ukumbusho kwa hiyo mikate, sadaka ya kusongezwa kwa BWANA kwa moto. 8 Kila siku ya Sabato ataipanga mbele za BWANA daima; ni kwa ajili ya wana wa Israeli, agano la milele. 9 Nayo itakuwa ya Haruni na wanawe; nao wataila katika mahali patakatifu; kwa sababu kwake ni takatifu sana katika sadaka zitolewazo kwa BWANA kwa moto, kwa amri ya milele. Kufuru na adhabu yake 10 Ikawa mwanamume mmoja ambaye mama yake ni Mwisraeli, na babaye ni Mmisri, alitokea kati ya wana wa Israeli akalikufuru; na kupigana na Mwisraeli katika kambi; 11 kisha huyo mwanamume ambaye mama ni Mwisraeli akakufuru jina la Bwana na kulaani nao watu wakampeleka kwa Musa. Mama yake mtu huyo alikuwa akiitwa Shelomithi, binti ya Dibri, wa kabila la Dani. 12 Nao wakamtia kifungoni, ili wapate kuambiwa neno litakalotoka kinywani pa BWANA. 13 Na BWANA akasema na Musa, na kumwambia, 14 Mtoe huyo aliyelaani nje ya kambi; na wale wote waliomsikia na waweke mikono yao kichwani mwake, kisha mkutano wote na wamwue kwa kumpiga kwa mawe. 15 Nawe nena na wana wa Israeli na kuwaambia, Mtu yeyote atakayemlaani Mungu wake atachukua dhambi yake. 16 Na yeyote atakayelaani jina la BWANA hakika atauawa; mkutano wote watamwua kwa kumpiga kwa mawe; kama ni mgeni, kama ni mzaliwa, hapo atakapolaani jina la BWANA atauawa. 17 Na mtu ampigaye mtu hadi akafa, lazima atauawa; 18 na atakayempiga mnyama hadi akafa atalipa; uhai kwa uhai. 19 Na mtu akimtia mwenziwe kilema; vile vile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo hivyo; 20 jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vile vile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo hivyo. 21 Na mtu amwuaye mnyama atalipa; na yeye atakayemwua binadamu atauawa. 22 Mtakuwa na sheria moja tu, kwa huyo aliye mgeni, na kwa mzalia; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. 23 Musa akanena na wana wa Israeli, nao wakamtoa huyo aliyeapiza nje ya kambi, wakamwua kwa kumpiga kwa mawe. Wana wa Israeli wakafanya kama BWANA alivyomwagiza Musa. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya