Walawi 17 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCUchinjaji wa wanyama 1 BWANA akamwambia Musa 2 Sema na Haruni, na wanawe, na wana wote wa Israeli, uwaambie; Neno hili ndilo aliloamuru BWANA, 3 Mtu yeyote wa nyumba ya Israeli atakayechinja ng'ombe, mwana-kondoo, au mbuzi, ndani au nje ya kambi, 4 wala hamleti mlangoni pa hema ya kukutania, kama matoleo kwa BWANA mbele ya hema ya BWANA; mtu huyo atahesabiwa kuwa ana hatia ya damu; amemwaga damu; na atatupiliwa mbali na watu wake; 5 ili wana wa Israeli walete sadaka zao, wazichinjazo mashambani, wazilete kwa BWANA, mpaka mlango wa hema ya kukutania, kwa huyo kuhani, ili wazichinje ziwe sadaka za amani kwa BWANA. 6 Naye kuhani atainyunyiza damu yake juu ya madhabahu ya BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania, na kuyateketeza mafuta yake, yawe harufu njema mbele za BWANA. 7 Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi. 8 Nawe utawaambia, Mtu yeyote katika nyumba ya Israeli, au miongoni mwa wageni, wanaokaa nao, atoaye sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, 9 wala haileti mlangoni pa hema ya kukutania, ili aisongeze kwa BWANA basi mtu huyo atatengwa na watu wake. Katazo la kula damu 10 Kisha mtu yeyote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yoyote, nitamkataa mtu huyo alaye damu, na nitamtenga na watu wake. 11 Kwa kuwa uhai wa mwili uko katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. 12 Kwa hiyo niliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aishiye kati yenu asile damu. 13 Mtu yeyote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu yake, na kuifunikia mchangani. 14 Kwa kuwa uhai wa kila kiumbe uko katika damu yake; ndio nikawaagiza wana wa Israeli, Msiile damu ya mnyama wa aina yoyote; kwa kuwa uhai wa kila kiumbe ni damu yake; yeyote atakayeila atatengwa. 15 Tena kila mtu atakayekula nyamafu, au nyama ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama, awe ni mzalia au mgeni, atafua nguo zake, na kuoga majini naye atakuwa najisi hadi jioni; ndipo atakapokuwa safi. 16 Lakini iwapo hazifui, wala haogi mwili, ndipo atakapolipizwa uovu wake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya