Walawi 15 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCMagonjwa ya zinaa 1 Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 2 Haya, semeni na wana wa Israeli, mkawaambie, Mtu yeyote atakapokuwa na kisonono na kutokwa usaha mwilini mwake, atakuwa najisi kwa ajili ya kisonono chake. 3 Na unajisi wake katika kisonono chake ni huu; kama mwili wake unachuruzika kisonono chake, au kama kisonono chake kimezuiwa mwilini mwake, ni unajisi wake. 4 Kitanda chochote akilaliacho mwenye kisonono kitakuwa najisi; na kitu chochote atakachokalia kitakuwa najisi. 5 Mtu yeyote atakayekigusa kitanda chake huyo, atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hadi jioni. 6 Na mtu atakayeketi katika kitu chochote alichokiketia mwenye kisonono, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hadi jioni. 7 Na mtu atakayegusa mwili wake mwenye kisonono atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hadi jioni. 8 Tena kama mwenye kisonono akimtemea mate mtu aliye safi; ndipo atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa ni najisi hadi jioni. 9 Na tandiko lolote atakalolipanda mwenye kisonono litakuwa najisi. 10 Mtu yeyote atakayegusa kitu chochote kilichokuwa chini yake huyo atakuwa najisi hadi jioni; na mtu atakayevichukua vitu vile atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hadi jioni. 11 Na mtu yeyote atakayeguswa na mwenye kisonono, ambaye hajanawa mikono yake majini, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hadi jioni. 12 Na chombo cha udongo ambacho amekigusa mwenye kisonono, kitavunjwavunjwa; na kila chombo cha mti kitaoshwa majini. 13 Na huyo aliye na kisonono atakapotakaswa na kisonono chake, atajihesabia siku saba kwa kutakaswa kwake, naye atazifua nguo zake; naye ataoga mwili wake katika maji ya mtoni, naye atakuwa safi. 14 Na siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, naye atakwenda mbele za BWANA mlangoni pa hema ya kukutania, naye atampa kuhani hao ndege; 15 na kuhani atawasongeza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho mbele za BWANA kwa ajili ya kisonono chake. 16 Na mtu yeyote akitokwa na shahawa yake, ndipo ataoga mwili wake wote majini, naye atakuwa najisi hadi jioni. 17 Na kila nguo au ngozi, ambayo ina shahawa, itafuliwa kwa maji, nayo itakuwa najisi hata jioni. 18 Huyo mwanamke ambaye mwanamume amelala naye kwa shahawa, wote wawili wataoga majini, nao watakuwa najisi hadi jioni. 19 Mwanamke yeyote aliye na hedhi, atatengwa kwa muda wa siku saba; na mtu yeyote atakayemgusa atakuwa najisi hadi jioni. 20 Na kitu chochote ambacho anakalia katika kutengwa kwake kitakuwa najisi; na kila kitu ambacho amekalia kitakuwa najisi. 21 Mtu yeyote atakayekigusa kitanda chake huyo mwanamke atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hadi jioni. 22 Mtu yeyote atakayekigusa chochote ambacho huyo mwanamke amekalia atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hadi jioni. 23 Kiwe ni katika kitanda, au chochote alichokikalia huyo mwanamke, atakapokigusa kitu hicho, atakuwa najisi hadi jioni. 24 Na mtu yeyote atakayelala na mwanamke na unajisi ukawa juu yake, atakuwa najisi muda wa siku saba; na kila kitanda alichokilalia kitakuwa najisi. 25 Na mwanamke kama akitokwa na damu yake siku nyingi, nayo si katika majira ya kutengwa kwake, au kama anatoka damu kuzidi majira ya kutengwa kwake; siku hizo zote za kutoka damu ya unajisi wake, atakuwa kama alivyokuwa katika siku za kutengwa kwake; yeye ni najisi. 26 Kila kitanda akilaliacho katika siku zote za kutoka damu kitakuwa kama kitanda cha kutengwa kwake; na kila kitu atakachokilalia kitakuwa najisi, kama unajisi wa kutengwa kwake. 27 Na mtu yeyote atakayevigusa vitu vile atakuwa najisi, naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hadi jioni. 28 Lakini huyo mwanamke akiwa ametakaswa na kule kutoka damu kwake, ndipo atakapojihesabia siku saba, na baadaye atakuwa safi. 29 Siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, na kumletea kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania. 30 Kuhani atamsongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA, kwa ajili ya kutoka damu ya unajisi kwake. 31 Ni hivi mtakavyowatenga wana wa Israeli na unajisi wao; ili wasife katika unajisi wao, hapo watakapoitia unajisi maskani yangu iliyo katikati yao. 32 Hii ndiyo sheria ya mwenye kisonono, na ya mtu ambaye shahawa yake inamtoka, akawa na unajisi kwa ajili yake; 33 na ya mwanamke ambaye yuko katika kutengwa kwake, na ya mtu ambaye ana kisonono, awe ni mwanamume, au ni mwanamke, na ya huyo alalaye na mwanamke mwenye unajisi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya