Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Waamuzi 9 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Abimeleki awania ufalme

1 Abimeleki, mwana wa Yerubaali, akaenda Shekemu kwa ndugu za mama yake, akanena nao, na wote waliokuwa wa nyumba ya baba ya mama yake, akasema,

2 Haya, neneni tafadhali masikioni mwa wanaume wote wa Shekemu, mkaulize, Je! Ni lipi lililo bora kwenu, kwamba hao wana wa Yerubaali wote, ambao ni watu sabini, wawatawale, au kwamba mtu mmoja awatawale? Tena kumbukeni ya kwamba mimi ni mfupa na nyama yenu.

3 Hao ndugu za mama yake wakanena habari zake masikioni mwa hao watu wote wa Shekemu maneno hayo yote; na mioyo yao ikaelekea kumwandama Abimeleki; kwa kuwa walisema, Huyu ni ndugu yetu.

4 Wakampa vipande vya fedha sabini vilivyotoka katika nyumba ya Baal-berithi, na kwa fedha hizo Abimeleki akaajiri watu wapuuzi mabaradhuli, wafuatane naye.

5 Kisha akaenda nyumbani kwa babaye huko Ofra, akawaua nduguze, hao wana wa Yerubaali, watu sabini, akawaua juu ya jiwe moja; lakini Yothamu, mwana mdogo wa Yerubaali, alisalia; kwa maana alijificha.

6 Kisha hao watu wote wa Shekemu wakakusanyika pamoja, na jamaa yote ya Milo, wakaenda na kumtawaza Abimeleki awe mfalme, karibu na huo mgandi ulio karibu na ngome iliyo katika Shekemu.


Mithali ya miti

7 Kisha walipomwambia huyo Yothamu, yeye akaenda, akasimama juu ya kilele cha kilima cha Gerizimu, akapaza sauti yake, akapiga kelele, na kuwaambia, Nisikieni mimi, enyi watu wa Shekemu, ili Mungu naye apate kuwasikia ninyi.

8 Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu yetu.

9 Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayumbayumbe juu ya miti?

10 Kisha miti ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu.

11 Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende nikayumbayumbe juu ya miti?

12 Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu.

13 Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayumbayumbe juu ya miti?

14 Ndipo hiyo miti yote ikauambia mti wa miiba, Njoo wewe, utawale juu yetu.

15 Huo mti wa miiba ukaiambia miti, Ikiwa kwa kweli mnanitia mafuta niwe mfalme juu yenu, basi njoni mkakae chini ya kivuli changu; la sivyo, na utoke moto katika mti wa miiba na kuiteketeza mierezi ya Lebanoni.

16 Basi sasa ikiwa mmetenda kwa nia njema na uzingativu, katika kumtawaza Abimeleki awe mfalme, na ikiwa mmemtendea mema Yerubaali na nyumba yake, na kumtendea kama ilivyostahili mikono yake;

17 (kwa maana baba yangu aliwatetea ninyi, na kuhatarisha uhai wake, na kuwaokoa na mikono ya Midiani;

18 nanyi mmeinuka juu ya nyumba ya baba yangu hivi leo nanyi mmewaua wanawe, watu sabini, juu ya jiwe moja, nanyi mmemtawaza Abimeleki, mwana wa kijakazi chake, awe mfalme juu ya watu wa Shekemu kwa sababu yeye ni ndugu yenu;)

19 basi ikiwa mmemtendea kwa nia njema na uzingativu Yerubaali na nyumba yake hivi leo, basi mfurahieni huyo huyo Abimeleki, yeye naye na awafurahie ninyi;

20 lakini ikiwa basi moto na utoke katika Abimeleki na kuwateketeza watu wa Shekemu, na jamaa ya Milo; kisha moto na utoke katika hao watu wa Shekemu, na katika jamaa ya Milo, na kumteketeza Abimeleki.

21 Kisha Yothamu akaenda zake na kukimbia, akaenda Beeri, na kukaa kuko, kwa kumwogopa Abimeleki nduguye.


Kuanguka kwa Abimeleki

22 Basi Abimeleki alitawala juu ya Israeli kwa muda wa miaka mitatu.

23 Kisha Mungu akatuma roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu; nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa udanganyifu;

24 ili kwamba huo udhalimu waliotendewa hao wana sabini wa Yerubaali ulipizwe, ili damu yao iwe juu ya Abimeleki ndugu yao, aliyewaua, na juu ya watu wa Shekemu, waliomtia nguvu mikono yake ili awaue hao nduguze.

25 Basi watu wa Shekemu wakaweka watu kumvizia juu ya vilele vya milima, ambao waliwapora watu wote waliopita njia hiyo karibu nao; naye Abimeleki aliarifiwa.

26 Kisha Gaali, mwana wa Ebedi, akaenda pamoja na nduguze, wakavuka na kufika Shekemu; na watu wa Shekemu wakawa na imani naye.

27 Nao wakatoka kwenda mashambani, wakavuna mashamba yao ya mizabibu, na kuzishindika hizo zabibu, na kufanya sikukuu, kisha wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala na kunywa na kumlaani huyo Abimeleki.

28 Naye Gaali mwana wa Ebedi akasema, Abimeleki ni nani, na sisi wa Shekemu ni nani, hata tukamtumikie yeye? Je, huyu mwana wa Yerubaali na Zebuli afisa wake hawakuwatumikia watu wa Hamori babaye Shekemu? Basi, kwa nini tumutumikie?

29 Laiti watu hawa wangekuwa chini ya mkono wangu! Hapo basi mimi ningemuondoa huyo Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki, Haya, ongeza jeshi lako, utokeze.

30 Basi hapo Zebuli, aliyekuwa mkuu wa mji, alipoyasikia hayo maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, hasira zake zikamwaka.

31 Naye akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, akasema, Tazama, Gaali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Shekemu; na wanaufitinisha mji huu kinyume chako.

32 Basi sasa, inuka wewe, usiku, wewe na watu walio pamoja nawe, mvizie mashambani;

33 kisha asubuhi na mapema, mara tu baada ya jua kuchomoza, inuka na uushambulie mji huo; na Gaali na wale watu walio pamoja naye watakapotokeza nje kupigana nawe, ndipo utakapowatenda kama utakavyoweza.

34 Basi Abimeleki na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka usiku na kuuvizia Shekemu kwa vikosi vinne.

35 Huyo Gaali mwana wa Ebedi akatoka nje, akasimama penye maingilio ya lango la mji; naye Abimeleki na hao watu waliokuwa pamoja naye wakainuka kutoka mahali pale walipokuwa wanavizia.

36 Basi Gaali alipowaona hao watu, akamwambia Zebuli, Tazama, watu washuka kutoka katika vilele vya milima. Zebuli akamwambia, Ni kivuli cha milima unachokiona kama ndio watu.

37 Kisha Gaali akasema mara ya pili, akanena, Angalia, watu washuka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kwa njia ya mwaloni wa Meonenimu.

38 Ndipo Zebuli akamwambia, Je! Kinywa chako sasa kiko wapi, hata ukasema, Huyo Abimeleki ni nani, hata inatupasa kumtumikia yeye? Je! Hawa sio majeshi hao uliowadharau wewe? Haya, toka nje sasa, tafadhali, upigane nao.

39 Basi Gaali akatokeza mbele ya watu wa Shekemu, akapigana na Abimeleki.

40 Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akakimbia mbele yake, wengi walijeruhiwa na kuanguka hadi kufikia maingilio ya lango la mji.

41 Abimeleki akakaa Aruma; naye Zebuli akawatoa Gaali na ndugu zake, wasikae katika Shekemu.

42 Ikawa siku ya pili yake, watu wakatoka waende mashambani; naye Abimeleki alipoambiwa.

43 Akawatwaa watu wake, na kuwagawanya katika vikosi vitatu, nao wakavizia mashambani; naye akaangalia, alipoona watu wakitoka nje ya mji, aliwashambulia na kuwaua.

44 Abimeleki, na vile vikosi vilivyokuwa pamoja naye, wakafululiza, wakasimama penye maingilio ya lango la mji, na vile vikosi viwili vikawarukia hao wote waliokuwa mashambani, na kuwaua.

45 Abimeleki akapigana na huo mji mchana kutwa; akautwaa mji, akawaua watu waliokuwamo ndani yake; kisha akauteketeza mji, na kuutia chumvi.

46 Kisha watu wote waliokaa katika ule mnara wa Shekemu waliposikia habari hiyo wakaingia ndani ya ngome ya nyumba ya El-berithi.

47 Abimeleki aliambiwa ya kuwa watu hao wote wa mnara wa Shekemu wamekusanyika pamoja.

48 Basi Abimeleki akakwea kwenda katika kilima cha Salmoni, yeye na wote waliokuwa pamoja naye; naye Abimeleki akashika shoka mkononi mwake, akakata tawi moja katika miti, akalishika na kujitwika begani mwake; akawaambia hao watu waliokuwa pamoja naye, “Haya, kile mlichoona nikifanya, nanyi fanyeni vivyo hivyo haraka”.

49 Basi watu hao wote wakakata kila mtu tawi lake, wakamfuata Abimeleki, wakayaweka hayo matawi pale ngomeni, na kuiteketeza moto hiyo ngome juu yao; ndipo watu wote wa huo mnara wa Shekemu wakafa, watu wapatao elfu moja, wanaume kwa wanawake.

50 Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akauzingira na kuutwaa.

51 Lakini ndani ya huo mji palikuwa na mnara wenye nguvu, na watu wote wanaume na wanawake wakakimbilia huko, na watu wote wa mji, nao wakajifungia ndani, wakapanda paa la mnara.

52 Abimeleki akauendea huo mnara na kupigana nao; naye akaukaribia mlango wa mnara ili auteketeze.

53 Na mwanamke mmoja akabwaga jiwe la kusagia la juu, nalo likampiga Abimeleki kichwani, na kulivunja fuvu la kichwa chake.

54 Ndipo akamwita kwa haraka huyo kijana aliyekuwa anamchukulia silaha zake, na kumwambia, Futa upanga wako, uniue, ili watu wasiseme juu yangu, Aliuawa na mwanamke. Basi huyo kijana wake akamchoma upanga, naye akafa.

55 Basi hapo watu wa Israeli walipoona ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaondoka wakaenda kila mtu mahali pake.

56 Kwa hiyo, Mungu akalipiza kisasi juu ya uovu wa Abimeleki aliomtenda baba yake, kwa kuwaua hao nduguze watu sabini;

57 uovu wote wa watu wa Shekemu Mungu alilipiza juu ya vichwa vyao; na hiyo laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawajia juu yao.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo